Habari Mseto

Polisi vidosho sasa marufuku kuvaa wigi

December 27th, 2019 1 min read

Na NICHOLSA KOMU

MAAFISA wa kike wa polisi watalazimika kuenda saluni ili kuondoa wigi zao za kuvutia punde sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya zitakapokamilika Januari 1, kwa mujibu wa agizo lililotolewa na Tume ya Huduma kwa Polisi (NPSC).

Agizo hilo linataka pia polisi wa kike Waislamu wakome kufunga hijabu za kimapambo, kwani wataruhusiwa tu kufunga za rangi nyeusi.

Idara ya polisi inasema kwamba siku hizi idara ya polisi inakosa heshima machoni pa umma kwani polisi wa kike wameamua kujirembesha kupita kiasi wakiwa kazini.

Kwa mujibu wa Naibu Inspekta Jenerali wa polisi, Bw Edward Mbugua, ambaye alitia sahihi agizo hilo, mienendo hiyo inayoibuka miongoni mwa polisi wa kike inaenda kinyume na maadili ya utendakazi wao.

“Wakati wa ziara yangu kwa muda wa wiki moja katika maeneo mbalimbali ya nchi, nimepata maafisa wa kike wa polisi wanaoshikilia vyeo mbalimbali wakiwa na mitindo isiyofaa ya nywele inayokiuka maadili ya kazi yao,” akasema Bw Mbugua.

Mkuu huyo wa polisi alidai kwamba baadhi ya mitindo ya kisasa ya nywele imewazuia hata maafisa hao wa kike kuvaa kofia zao vyema kichwani wakiwa kazini.

“Hili halikubaliki kamwe kwenye maadili yao ya utendakazi,” akaongeza.

Afisa huyo pia alizua maswali kuhusu vazi la hijabu lenye rangi mbalimbali kwa polisi wa kike Waislamu, akisisitiza kuwa wanafaa kuvaa ya rangi nyeusi pekee jinsi ilivyo kwenye agizo la idara hiyo.

“Polisi wa kike Waislamu wamepuuza hijabu nyeusi inayokubaliwa na sasa wanavaa za rangi mbalimbali. Wanafaa wakome na kufuata sheria,” akasema.

Makamanda wa polisi wanatarajiwa kutekeleza amri hiyo na kuhakikisha kuwa polisi wa kike wenye mtindo wa nywele usiofaa wanatii na kuondoa urembeshaji huo kufikia Desemba 31.

Tume hiyo pia ilishikilia kwamba polisi wote lazima wakumbatie sare mpya ya polisi na mavazi ya kinadhifu, amri ambayo makamanda wote wa polisi watahakikisha inatekelezwa vilivyo.