Uncategorized

Polisi wa Kenya kule Haiti wataka helikopta, magari mazito na manuwari ya kivita

Na NYABOGA KIAGE August 20th, 2024 2 min read

POLISI wa Kenya kule Haiti sasa wanataka silaha zaidi, manowari ya kivita pamoja na helikopta kusaidia kutimiza malengo yao ya kumaliza magenge nchini humo.

Duru wikendi ziliarifu Taifa Leo kuwa kikosi cha Kenya chini ya kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa (UN), kinatatizwa na ukosefu wa silaha na vifaa vingine hatari vya kivita.

“Hadi sasa, tumefaulu kukabiliana na magenge hayo ila tatizo ni silaha za kivita,” afisa wa ngazi ya juu ambaye ni sehemu ya kikosi kinachoendesha operesheni kikaeleza Taifa Leo.

Mnamo Julai 6, polisi wa Kenya walipokea silaha za kivita ikiwemo magari kutoka Marekani ila gari moja lishaharibiwa na magenge yaliyoendesha uvamizi wa kushtukiza dhidi yao.

Gari moja nalo limeandamwa na tatizo la kiufundi baada ya kulipuliwa na bomu lililotegwa ardhini mji wa  Gauthier, Haiti. Wakati wa kisa hicho polisi Wakenya walikuwa wakikabiliana na magenge yaliyokuwa yamechukua usimamizi wa mji huo.

Mji wa Gauthier ndio hutumika kuelekea nchi jirani ya Jamuhuri ya Dominican. Magari ya kivita yaliyotolewa na Marekani pia yalikuwa yakitumika kuwasafirisha polisi na vifaa vya kivita wakati wanapoendeleza operesheni za kutwaa sehemu zinazodhibitiwa na magenge hatari.

Kenya ni kati ya nchi ambazo zimetoa maafisa wake wa usalama ili washirikiane na polisi wa Haiti kuwakabili magenge.

Hata hivyo, mataifa ya Jamaica na Bahamas bado yanafuatilia jinsi hali ilivyo Haiti kabla ya kuwatuma polisi wao katika nchi hiyo inayoelekea kusambaratishwa na mapigano kati ya serikali na magenge hatari.

Kamanda Mkuu anayesimamia operesheni Haiti Godfrey Otunge Jumatatu alisema ujumbe wa watu saba kutoka Bahamas na Jamaica ulizuru Haiti na utaweka wazi ni lini watatuma maafisa wao wa usalama kupiga jeki kikosi cha Kenya.

“Ujio wa polisi kutoka Jamaica utafahamika baada ya ujumbe uliotumwa kumaliza kutathmini jinsi hali ilivyo,” akasema Bw Otunge.

Ujumbe wa Jamaica uliongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Saint Lucia Dkt Kenny Anthony na waziri mkuu wa zamani wa Jamaica Bruce Holding, uliandaa mkutano na Bw Otunge katika hoteli ya Montana inayopatikana Petion Ville, Haiti.

Bw Otunge alisema kuwa ujumbe huo hasa ulitaka kufahamu jinsi vikosi vya usalama vimekuwa vikifanya kazi na changamoto ambazo vimekumbana nazo.

“Walitaka hasa kujua baadhi ya matatizo yanayotuzonga hasa yale ambayo yanahitaji suluhu za dharura ili nchi nyingine nazo zitume maafisa wao wa usalama kuongeza idadi yetu hapa,” akasema Bw Otunge.

Katika kikoa hicho, inaaminika kuliibuka malalamishi kuhusu kucheleweshwa kwa silaha za kivita, vifaa na magari. Bw Otunge hasa alisema polisi wanahitaji ndege aina ya helikopta kuwasaida kwenye operesheni dhidi ya magenge.

Kando na Kenya, Jamaica na Bahamas, mataifa mengine ambayo yanatarajiwa kutuma vikosi vyao Haiti ni Benin, Belize, Barbados, Antigua na Barbuda.

Nyingine ni Bangladesh, Algeria, Ufaransa, Ujerumani, Trinidad na Tobago. Uturuki, Uingereza na Uhispania. Baraza la Shirika la Umoja wa Kimataifa Kuhusu Usalama (UN) mnamo Oktoba 2023 liliidhinisha polisi Wakenya kuendeleza operesheni Haiti.

Baraza hilo lilitaka walinda usalama wahakikishe hawakiuki au kuvuruga haki za kibinadamu na pia wahakikishe kuwa operesheni hiyo inaendeshwa kulingana na sheria za kimataifa.

Hadi sasa, polisi 396 wamepelekwa kule Haiti huku Kenya ikitarajiwa kuwatuma wengine 600 zaidi japo Bw Otunge alisema kuwa bado haijabainika ni lini polisi hao wa ziada watatumwa.

-Imetafsiriwa na CECIL ODONGO