Habari Mseto

Polisi wa kike akamatwa kwa madai ya kumkatakata wakili mikono

October 9th, 2020 1 min read

PIUS MAUNDU Na BENSON MATHEKA

POLISI katika Kaunti ya Makueni wamemkamata mwenzao mwanamke anayedaiwa kumkata mikono wakili mmoja mjini Wote.

Afisa huyo aliyetambuliwa kwa jina Nancy Njeri, alikamatwa kufuatia kisa ambacho wakili Onesmus Masaku alikatwa mikono yote miwili akiwa nyumbani kwake.

Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Makueni, Timothy Maina alisema afisa huyo atashtakiwa kwa kujaribu kuua.

“Kufuatia kisa ambacho wakili mmoja kwa jina Onesmus Masaku anayehudumu katika Mahakama ya Makueni alijeruhiwa vibaya na Konstebo wa polisi Nancy Njeri, afisa huyo amekamatwa na atafikishwa kortini kushtakiwa kwa kujaribu kuua,” alisema Bw Maina.

Ripoti ya polisi ilisema afisa huyo aliripoti kwamba Bw Masaku alimwalika katika nyumba yake mjini Wote mnamo Jumatano usiku na akataka wafanye mapenzi, na alipokataa wakili huyo akajaribu kumlazimisha.

“Aliripoti kuwa wakili huyo alimshika na kumsukuma akimlazimisha aingie chumba cha kulala. Hii ilimfanya afisa huyo kuchukua upanga na akamkata mikono yote miwili kabla ya kutoroka,” Bw Maina alieleza.

Wakili huyo alipelekwa katika hospitali ya Kaunti ya Makueni kabla ya kuhamishwa hadi Hospitali Kuu ya Kenyatta jijini Nairobi akiwa katika hali mbaya.

Bw Maina alisema afisa huyo alipata jeraha katika sikio la upande wa kulia alilodai aliumwa na wakili huyo.

Katika kisa tofauti, polisi mjini Malindi wanachunguza kisa ambapo askari mwanamke wa magereza alipatikana amejitia kitanzi.

Kulingana na naibu chifu wa eneo hilo Renson Baya, afisa huyo ambaye alikuwa akihudumu katika gereza la Manyani alipatikana nyumbani kwake katika kijiji cha Mgurureni, kata ya Mida.

Inaarifiwa kuwa afisa huyo ambaye pia ni mama wa watoto wawili alikuwa kwenye likizo kisa hicho kilipotendeka.

Bw Baya alisema simu ya mwanamke huyo ilikuwa imezimwa alipopatikana akiwa amejinyoga kwa kutumia kipande cha leso.