Kimataifa

Polisi wa kike waagizwa kuvalia suruali fupi kuvutia watalii

July 19th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

BRUMMANA, LEBANON

POLISI wa trafiki wa kike wameagizwa wawe wakivaa suruali fupi ili kuvutia watalii mjini Brummana, Lebanon.

Ripoti zinasema agizo hilo lilitolewa na Meya wa mji huo Pierre Achkar, kwa minajili ya kuvutia watalii wanaotoka katika mataifa ya Magharibi.

Mashirika ya habari yalimnukuu kusema alichukua hatua hiyo baada ya kutambua jinsi watalii wenyewe hupenda kuvaa suruali fupi.

Picha zilizosambazwa na mashirika ya habari zilionyesha polisi wa trafiki wa kike wakiwa wamefuata maagizo hayo ya Meya.

Walivaa suruali fupi mno ambazo zilifunika sehemu ndogo tu ya mapaja.

Baadhi ya wakazi walimkashifu meya kwa kutoa agizo hilo ambalo wakosoaji wanaamini ni kudhalilisha hadhi ya wanawake katika jamii.

Kulingana nao, hatua hiyo ni sawa na kudharau utaalamu wa polisi wa kike na badala yake kuwachukulia kama viumbe vya ngono visivyostahili heshima.

Wengine walisema haifai mji huo utupilie mbali desturi zake za unadhifu na kuiga mienendo ya mataifa ya Magharibi isiyoenda sambamba na maadili yao ya kijamii.

-Imekusanywa na Valentine Obara