Habari za Kitaifa

Polisi wa ngazi za juu wa zamani King’ori Mwangi afariki akipokea matibabu

February 11th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Inspekta Jenerali wa Polisi wa zamani, Bw King’ori Mwangi, ameaga dunia.

Kwenye taarifa, familia yake ilisema kuwa marehemu alifariki Jumapili katika hospitali moja jijini Nairobi, alikokuwa amelazwa.

“Tungetaka kuufahamisha umma kuhusu kifo cha Bw King’ori Mwangi, afisa wa polisi mstaafu. King’ori alifariki leo [Jumapili] asubuhi katika hospitali moja, Nairobi, alikokuwa akipokea matibabu. Familia itaueleza umma kuhusu mipango ya mazishi,” ikaeleza taarifa hiyo.

Alifariki kutokana na matatizo yanayohusiana na upasuaji wa kimatibabu.

Marehemu alihudumu kama Mkuu wa Polisi wa Mkoa katika maeneo ya Nairobi, Mombasa na Magharibi.

Pia, alihudumu kama Mkurugenzi wa Mikakati katika makao makuu ya polisi, Msemaji wa Polisi, Mkurugenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Polisi mjini Kiganjo na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi.

Maafisa wenzake walimwomboleza kama mtu aliyejitolea, aliyekuwa mkakamavu daima kwenye kazi yake.

“Alikuwa mtu mzuri. Tunamwomba Mungu amweke mahali pema peponi,” akasema polisi mmoja wa ngazi za juu.

Alistaafu kutoka Idara ya Polisi mnamo 2021 baada ya kufikisha umri wa kustaafu.