Habari Mseto

Polisi wachunguza ajali iliyoua watu wanne

March 24th, 2024 1 min read

NA GEORGE MUNENE

POLISI wanachunguza kilichosababisha ajali iliyoua watu wanne kwenye barabara ya Gatuto- Baricho, Kaunti ya Kirinyaga.

Wengine kadhaa walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyotoka mnamo Jumamosi jioni, Machi 23, 2024 na kukimbizwa katika hospitali ya Kerugoya kwa matibabu.

Ajali hiyo ilihusisha matatu iliyokuwa ikielekea Baricho kutoka Kagio, ambapo ilianguka na kubingiria.

Kamanda wa polisi Kaunti ya Kirinyaga Andrew Naibei alithibitisha ajali hiyo na kusema uchunguzi unaendelea.

“Matatu ilianguka tu na kubingiria na tunataka kujua kilichofanyika,” alisema Bw Naibei, akiongeza kuwa dereva alikuwa akitumia njia fupi kuelekea Baricho.