Polisi wachunguza kisa cha mwanafunzi wa Kidato cha Nne kujitia kitanzi

Polisi wachunguza kisa cha mwanafunzi wa Kidato cha Nne kujitia kitanzi

BENSON MATHEKA Na CORNELIUS MUTISYA

MAAFISA wa polisi eneo la Kathiani, Kaunti ya Machakos, wanachunguza kisa ambacho mvulana mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Kaewa, alipatikana amejitia kitanzi nyumbani kwa wazazi wake.

Mwili wa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 22, ulipatikana ukining’inia kutoka paa la nyumba saa chache baada yake kutoka shule Jumatano jioni.

Kulingana na naibu wa chifu wa kata ndogo ya Kalunga, lokesheni ya Kaewa, Bw Bonface Kiilu, mwanafunzi huyo hakuacha ujumbe kueleza sababu za kujitoa uhai.

“Inasikitisha mwanafunzi aliyekuwa mwerevu alijitoa uhai. Uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kilichomfanya achukue hatua hiyo,” Bw Kiilu aliyeandamana na maafisa wa polisi kuondoa mwili aliambia Taifa Leo.

Afisa huyo wa utawala alihimiza wanafunzi kuzungumza na wazazi wao, walimu na viongozi wa kidini wanapopata matatizo badala ya kuchukua hatua zinaweza kuwaweka kwenye hatari.

“Kisa hiki ni cha kwanza kutokea eneo hili na ni pigo sio kwa familia mbali kwa jamii,” alisema.

Bw Kiilu aliwataka wanafunzi kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na tabia zinazoweza kuharibu maisha yao ya siku zijazo.

“Wazazi wanafaa kurahisisha mawasiliano na watoto wao ili waweze kufahamu wanayopitia katika maisha yao,” alisema.

Mwili wa mwanafunzi huyo unahifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Machakos.

  • Tags

You can share this post!

Sheffield United yaduwaza Manchester United ligini kwa...

Burnley watoka nyuma na kunyima Aston Villa fursa ya...