Polisi wachunguza Mbogo kwa madai ya uchochezi

Polisi wachunguza Mbogo kwa madai ya uchochezi

NA WINNIE ATIENO

POLISI katika Kaunti ya Mombasa wamesema wanamchunguza Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo, kwa madai ya uchochezi.

Bw Mbogo ni mgombea mwenza wa aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kwa shindano la ugavana Mombasa kupitia kwa tiketi ya Wiper.

Hayo yaliibuka huku wanasiasa wakionywa dhidi ya matamshi ya uchochezi wakati nchi inapoelekea kwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Kamishna wa kaunti ya Mombasa, Bw John Otieno, alidai kuwa mbunge huyo amerekodiwa akitoa matamshi ya uchochezi wakati wa kampeni zake.

“Msiwagawanye watu kulingana na kabila, sote ni Wakenya. Ubaguzi wa aina hiyo ni hatari sana. Nawaomba wanasiasa wakome siasa za uchochezi. Lakini tunafuatilia mienendo ya kila mwanasiasa na matamshi wanayotoa ili tuhakikishe amani inadumu Mombasa,” alisema Bw Otieno.

Hata hivyo, mbunge huyo alipinga madai hayo akisema yeye haenezi ukabila na wala hajawahi kuchochea wananchi kwa misingi ya kikabila.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Mbogo alisema amekuwa mstari wa mbele kukabiliana na matapeli wanaovuruga uchumi wa Mombasa na wale wanaofuja mali ya umma na hayo ndiyo yamekuwa msingi wa kampeni zake.

Aliashiria huenda anaandamwa kwa sababu ya misimamo yake ya kisiasa.

Vile vile, mbunge huyo alisema hajapokea taarifa yoyote kutoka kwa idara ya usalama kuhusu mashtaka dhidi yake.

“Sijawahi kutamka maneno ya uchochezi, lini? Au wapi? Hizo ni propaganda tu. Hakuna mambo ya ukabila Pwani, sote ni kitu kimoja. (Wapinzani wetu) wameingia uoga kwa sababu mimi na mgombea mwenzangu wa ugavana, Bw Sonko, tumeanza kuwapeleka mbio,” akasema Bw Mbogo.

Wakati uo huo, Bw Otieno alisema maafisa wa usalama wanaendelea kuchunguza wanasiasa wengine wanaotoa matamshi ya uchochezi.

Bw Otieno alisema wanasiasa hao wataitwa na polisi kuandikisha taraifa kamili hivi karibuni.

Asasi za usalama pia zilitoa tahadhari kwa baadhi ya wanasiasa wanaosajili vijana kujiunga na makundi ya uhalifu ambavyo nia yao ni kuwatia hofu wapiga kura wakati wa uchaguzi ili kususia zoezi hilo.

Wakuu wa usalama, walifichua kuwa kikosi maalumu cha polisi kimeanza kushika doria sehemu ambayo inakadiriwa kuwa hatari ikiwemo Likoni, Mji wa Kale, Kisauni na Nyali.

Maafisa hao wanaendelea kushika doria katika maeneo yenye utovu wa usalama ili kupata habari kuhusu utumizi wa dawa haramu za magenge ya wahalifu kuzua rabsha kwenye mikutano.

“Hatutakubali uhalifu Mombasa. Tutakabiliana na wanasiasa wanaoendelea kugawanya wakenya na kuzua siasa za ukabila, hakuna mpwani na mbara sote ni wakenya. Lazima kuwe na uchaguzi wa amani,” alisema Bw Otieno.

Bw Otieno alisema Mombasa ni jiji muhimu sana ambalo linategemea utalii hivyo basi usalama lazima udhibitiwe na amani idumishwe.

“Kama hatutaweka mikakati ifaayo ya usalama tutawafukuza wawekezaji na watalii,” akasema Bw Otieno.

Kaunti ya Mombasa imeshuhudia cheche za siasa huku wanasiasa wakiendeleza kampeni zao.

  • Tags

You can share this post!

BURUDANI: Mwigizaji mahiri na mwalimu wa Kifaransa

Shofco Mathare yaota mizizi ikilenga kupanda daraja

T L