Makala

Polisi wadaiwa kutumia vitisho kubugia pombe ya bure kwa baa

May 9th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

WAUZAJI wa pombe waliopewa leseni kuhudumu wametoa malalamishi kwamba kuna maafisa wa polisi wafisadi katika Kaunti ya Murang’a ambao kazi yao ni kufanya misako ndani ya baa huku nia yao ikiwa ni kujipa pombe ya bure na kuitisha hongo.

Katika visa kadhaa ambavyo vimekusanywa na kamati ya kiusalama inayoongozwa na Kamishna wa Kaunti Joshua Nkanatha, mtandao huo unashirikisha polisi watundu wa kujitakia vya bwerere.

Kisa kimoja kati ya vingi vilivyonakiliwa ni cha Aprili 26, 2024, ambapo msako ulifanywa katika baa ya Central iliyoko mjini Murang’a.

“Maafisa walifika na wakatia mbaroni wahudumu wawili wa kike pamoja na wateja kadhaa na kisha wakapelekwa katika kituo cha polisi cha Murang’a,” taarifa hiyo rasmi ambayo imenakiliwa kama kisa MUR11965657 yakariri.

Ukora ni kwamba, afisa mmoja ameripotiwa kwamba alimtoa mshukiwa mmoja kwa seli za polisi na kisha akarejea naye hadi kwa baa na ambapo alimshurutisha kumpa Sh10,000 zilizokuwa za mauzo kama hongo ya kuachiliwa (kwa mshukiwa huyo).

Nao wateja walidaiwa kujinunulia uhuru wao kivyao, hali ambayo inaashiria kutumika kwa stesheni za polisi kama mamlaka haramu ya ukusanyaji ushuru au mahakama bandia za kutoza washukiwa faini, sawa na genge la Mungiki ambalo linafahamika vyema kwa kudai ushuru bandia dhidi ya wenyeji.

“Kando na kunyima serikali kuu ushuru kupitia mikakati ya haki ambapo washukiwa wangepigwa faini halali mahakamani, kile kilifanyika katika kisa hiki ni ufisadi wa wazi,” ripoti hiyo yasema.

Aidha, ile pombe ambayo ilikuwa imetwaliwa kutoka kwa baa hiyo haikurejeshwa.

Wamiliki wa baa walioongea na Taifa Leo wamedai kwamba mara nyingi ni kawaida polisi kukatalia pombe ambayo wanachukua wakati wa misako.

Mmoja wa wamiliki wa baa aliambia Taifa Leo kwamba kuna maafisa ambao hutembea wakiwa kwa ‘genge la watatu’ ambao wakiingia ndani ya baa, huitisha pombe hata ya Sh2,000 na wakimaliza kunywa wanasema bili ni ya mwenye baa la sivyo ajiandae kukamatwa ambapo atadaiwa hongo au faini ya zaidi ya Sh50,000.

Ni hali ambayo imewakera baadhi ya wamiliki, ripoti hiyo ya kiusalama katika kisa kingine ambacho kimenakiliwa kama MUR3803796 ikifichua baadhi ya waathiriwa wakiteta kwa kamati ya kiusalama kwamba wataandaa orodha ya uvamizi wa baa na maafisa ambao hudai wametumwa na makamanda wa polisi.

Wanateta katika ujumbe huo wao kwamba ni ama polisi watujulishe shida yao huwa ni gani.

“Kando na kuwapa Sh100 kwa siku kwa kila baa, wakitukamata huwa bado wanatudai hongo ya hadi Sh10,000 na hatimaye kukatalia pombe yetu ambayo huwa wamebeba katika misako hiyo,” akasema mlalamishi katika ripoti hiyo.

Wamiliki hao katika barua yao wamewataka polisi waamue kama nia yao ni pombe ya bure, hongo au vyote viwili ili ijulikane rasmi msimao ni wao ni upi.

Ripoti hizo za wamiliki wa baa hata zinataja baadhi ya maafisa ambao wamekuwa kero kuu kwao, wakimtaka Bw Nkanatha atekeleze mikakati ya kuwazima kutandaza ufisadi huo wao ambao huumiza biashara.

Hali hii imekuwa ikizingatiwa sana na Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye mara kwa mara amekuwa akionya maafisa wa polisi.

“Vita dhidi ya ulevi kiholela na mihadarati huathiriwa pakubwa na ufisadi wa baadhi ya maafisa wa polisi,” husema Bw Gachagua.

Naibu Rais amekuwa akiwataka polisi kuzingatia uadilifu kazini huku serikali ikipambana kuwaimarishia masilahi yao ya mishahara “ndio nasi tukiwapa kitu kikubwa, nanyi mkome haya mambo ya kudai kitu kidogo”.

Bw Gachagua aidha amekuwa akionya kwamba yule ambaye atalemewa na kazi ajue kwamba hatakuwa akipewa uhamisho wa kwenda kuhudumia wengine kwa kuwa hilo ni sawa na kuhamisha shida ikawaathiri wengine.

“Tutakuwa tunawafuta kazi maafisa hao wazembe, watundu na wafisadi katika stesheni ambazo wanahudumia kwa wakati huo wa kukadiriwa kuwa hawafai,” akasema Bw Gachagua.