Habari Mseto

Polisi wadandia ufichuzi wa sakata ya uuzaji watoto

November 18th, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA na RICHARD MUNGUTI

SIKU chache baada ya Shirika la Habari la BBC kufichua biashara ya uuzaji wa watoto iliyonoga jijini Nairobi, polisi sasa wanadai kwamba ni wao waliogundua na kuvunja mtandao wa walanguzi wa watoto.

Kwenye makala ya upekuzi yaliyopeperushwa na shirika hilo kupitia kipindi cha BBC African Eye, maafisa wa afya katika hospitali ya Mama Lucy na kliniki kadhaa za kibinafsi katika mitaa ya Nairobi walianikwa wakiuza watoto wanaotelekezwa au wanaozaliwa na wanawake wasio na uwezo wa kuwalea kama vile vijana wanaorandaranda mitaani. Makao ya watoto mayatima pia yalitajwa kwa kufanikisha biashara ya watoto.

Kabla ya ufichuzi huo, biashara hiyo ilikuwa imeendelea kwa muda bila maafisa wa usalama kugundua na kuwachukulia hatua wahusika.

Ni baada ya ufichuzi huo ambapo polisi waliwakamata washukiwa watatu wafanyakazi wa hospitali ya Mama Lucy.

Lakini kwenye taarifa aliyotoa jana, Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Nzioki Mutyambai alisema kwamba ni polisi waliofichua biashara hiyo ya ulanguzi wa watoto jijini Nairobi.

Bila kutaja makala hayo au mchango wa wanahabari waliowekeza nguvu, rasilmali na kuhatarisha maisha yao kufanya upekuzi wa kina, Bw Mutyambai alisema polisi walivunja biashara hiyo kufuatia habari kutoka kwa washirika wao.

Taarifa ya Bw Mutyambai ilisema kwamba polisi walifanya operesheni ya kufichua biashara hiyo haramu ya ulanguzi wa watoto.

“Wakati wa operesheni ya polisi kufichua uhalifu huo, polisi walibaini kuwa hospitali za umma na makao ya watoto yalihusika,” alisema Bw Mutyambai.

Kufuatia ufichuzi wa BBC, maafisa watatu wakuu wa hospitali ya Mama Lucy akiwemo Afisa Mkuu Mtendaji, Dkt Emma Mutio na Afisa Msimamizi, Regina Musembi walikamatwa.

Mfanyakazi wa mashuriano ya kijamii wa hospitali hiyo, Bw Fred Leparan ambaye mchango wake uliangaziwa katika makala hayo pia alikamatwa.

Hakimu Mwandamizi, Bw Bernard Ochoi aliamuru watatu hao wazuiliwe hadi leo atakapoamua ikiwa atawaachilia kwa dhamana ama atawazuia kwa siku 10 kama alivyoombwa na afisa wa polisi Inspekta Wanga Masake anayechunguza kesi hiyo.

Ombi la kuwazuilia siku 10 lilipingwa vikali na wakili Danstan Omari aliyesema madaktari hao wakuu walianza kufanya kazi hospitalini humo siku 10 zilizopita na kamwe hawakuhusika.

Hata hivyo, polisi walisema kwamba ni uchunguzi na operesheni waliyofanya iliyochangia kukamatwa kwa washukiwa hao.

“Wakati wa uchunguzi na operesheni, ilibainika kwa masikitiko kwamba maafisa wakuu wa hospitali moja ya umma kwa ushirikiano na walanguzi wa watoto walihusika. Kufikia sasa, maafisa watatu wakuu wa afya wamekamatwa,” Bw Mutyambai alisema.

Aliagiza makamanda wa polisi wa kaunti zote kushirikiana na Idara ya watoto kukabiliana na kuzuia ulanguzi wa watoto. Kulingana na Bw Mutyambai, maafisa hao watakuwa wakifanya uchunguzi kuhusu visa vinavyohusu watoto hasa katika hospitali za umma, za kibinafsi na makao ya watoto katika kaunti zao.

Alihimiza umma kutoa habari kuhusu visa vya wizi wa watoto kwa maafisa wa polisi na wa idara za serikali zinazohusika ili kusaidia kukabiliana na wahalifu.

Alihakikishia umma kwamba habari watakazotoa zitawekwa kuwa siri.

Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i alimsifu Bw Mutyambai “kwa kuchukua hatua za haraka.”