Polisi wakamata washukiwa 81 na kutwaa silaha hatari Mtwapa

Polisi wakamata washukiwa 81 na kutwaa silaha hatari Mtwapa

Na WACHIRA MWANGI

POLISI katika eneo la Mtwapa kaunti ya Kilifi wamewatia mbaroni watu 81 baada ya kupatikana wakiwa wamekusanyika kinyume na sheria na kudaiwa kuwa na nia ya kutekeleza uhalifu.

Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Kilifi Kusini Bw Mohamed Wako, alieleza kuwa watu hao, wanawake watano na wanaume 76, walikamatwa katika nyumba moja iliyoko katika mtaa wa Golden Key, eneo la Mtomondoni.

Bw Wako alieleza kuwa maafisa wa polisi walipata ripoti kutoka kwa umma. Walielekea kwenye eneo la tukio, ambapo waliwakuta watu hao wakila viapo.

“Tunawashukuru sana wakazi kwa kumakinika. Walitupatia habari zilizotuwezesha sisi kama taasisi za usalama. Hatua ya haraka tuliyoichukua, ilituwezesha kuwanasa wakila viapo,” alisema Bw Wako.

Bw Wako alihoji kuwa polisi wanafanya uchunguzi, kubaini sababu kamili ya mkusanyiko wa watu hao. Kulingana na askari, watu hao walikuwa wakiapa huku wamebeba silaha.

Baadhi ya vitu vilivyopatikana katika eneo la Golden Key, Mtomondoni mjini Mtwapa ambapo watu 81 people walikamatwa Juni 29, 2022. PICHA | NMG

Polisi walikusanya zaidi ya panga 30, visu na vitu vingine vilivyotumika kula kiapo.

Taarifa zinaonyesha kuwa watu kadhaa kati ya walioshikwa walitoka maeneo ya Rabai, Kilifi na Kwale.

Bw Wako alieleza kuwa, hawangetambua iwapo watu hao walikuwa katika kundi linalojiita Mombasa Republican Council (MRC), ila walikuwa na uhakika kuwa lengo lao halikuwa zuri.

Polisi waliwaomba wakazi waendelee kuwa macho, ili wafahamu yanayofanyika katika mitaa yao.

Watu hao watafikishwa katika mahakama ya Shanzu, kujibu mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

Wakuu wa Bhadala Jamat walaani vurugu zilizotokea katika...

Mwaniaji ugavana Kiambu aitaka serikali ihakikishe Wakenya...

T L