Habari

Polisi wakamata washukiwa watatu wa genge la uvamizi Bamburi

August 6th, 2019 1 min read

Na MOHAMED AHMED

WASHUKIWA watatu wa genge ambalo Jumatatu usiku liliwashambulia wakazi wa baadhi ya maeneobunge ya Kisauni na Nyali mjijni Mombasa wamekamatwa.

Washukiwa hao watatu walitambuliwa kama Jackson Okelo, 26, Paul Ayub, 18, na mwingine mwenye umri wa miaka 17.

Maafisa wa polisi waliwakamata watatu hao wakati wa msako mkali baada ya genge kuwashambulia wakazi Jumatatu usiku ambapo raia 13 walipata majeraha.

Wanne wako katika hali ambayo si nzuri sana kiafya na wanatibiwa katika Coast General Hospital.

Kamanda wa polisi katika Kaunti ndogo ya Kisauni, Julius Kiragu amesema washukiwa wa uhalifu huo walipatikana na bidhaa ambazo ni mali ya majeruhi wa shambulizi.

“Washukiwa ambao wamekamatwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kadzandani na watapandishwa kizimbani katika Mahakama ya Shanzu,” Kamanda Kiragu ameambia Taifa Leo akihojiwa kwa simu.

Uhalifu huo wa usiku ulisitisha shughuli na kuibua hali ya taharuki katika eneo la Bamburi Mwisho.