Habari Mseto

Polisi wakana kushirikiana na wanamgambo wa Al-Shabaab

February 5th, 2019 2 min read

NA BRUHAN MAKONG

POLISI mjini Wajir wamekanusha madai kwamba wanashiriki biashara haramu na kundi la kigaidi la Al Shabaab kisha kuwaruhusu kuingia nchini baada ya kulipwa fedha.

Madai hayo yalizuka baada ya ripoti kuenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanajeshi wa Kenya(KDF) walikuwa wakiwalaumu polisi kwa kutatiza juhudi zao za kupigana na ugaidi.

Kiini cha uhasama kati ya polisi na KDF ni magunia kadhaa ya sukari yaliyoingizwa nchini kiharamu na kunaswa na KDF, kisha yakakabidhiwa polisi wa kituo cha Habaswein na baadaye yakadaiwa kupotea katika hali tatanishi.

Mtu asiyejulikana alidai kwamba OCPD wa kituo hicho alikuwa akiuza sukari hiyo kwa Alshabaab akitumia gari la polisi kisha kufaulisha uvamizi wao nchini, hatua inayowagonganisha na KDF wanaojitahidi usiku na mchana kulitokomeza kundi hilo nchini.

Hata hivyo, OCPD wa Habaswein Benjamin Kimwele ambaye anahusishwa na ufisadi huo amekanusha madai hayo na kusema yanalenga kuharibu uhusiano mzuri kati ya polisi na maafisa wa KDF.

Afisa huyo hata hivyo alimlaumu afisa wa cheo cha chini kutoka idara nyingine ambaye alipewa uhamisho hadi kituo kingine majuma mawili yaliyopita kutokana na ukosefu wa nidhamu baada ya malalamishi kutoka kwa umma kwa kueneza habari hizo.

Bw Kimwele alidai kwamba hatua yake ya kufanikisha uhamisho wa afisa huyo ndiyo imezua kisasi na kuenezwa kwa habari feki dhidi yake ili kumharibia kazi.

Aliongeza kwamba msimamo wake mkali katika vita dhidi ya ugaidi huenda umewakasirisha baadhi ya maafisa wenzake ambao sasa wanamlimbikizia kila maovu ili ahamishwe kutoka kituoni humo.

“Kwa muda wa mwaka mmoja uliopita tangu nitue hapa, nimelihudumia taifa langu kwa moyo mkunjufu na wema unaofaa haswa katika kufanikisha vita dhidi ya ugaidi,”

“Madai kwamba nimekuwa nikishirikiana na magaidi hayana msingi ila yanalenga kuharibu jina langu. Nilizuia vijana watano waliokuwa wakitorokea Libya kujiunga na makundi ya kigaidi kati ya hatua nyingine nyingi ya kutokomeza ufisadi,” akaongeza huku akishikilia kwamba magunia hayo bado yapo kituoni humo yakisubiri kuharibiwa na maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru(KRA).

Kamanda Mkuu wa Polisi Kaunti ya Wajir Stephen Ng’etich alithibitisha kwamba ametembelea kituo hicho na kupata kwamba magunia yote 309 ya sukari hiyo hayajaguswa.