Makala

Polisi walia kupunjwa fedha zao za sacco

February 28th, 2024 2 min read

WANDERI KAMAU Na NYABOGA KIAGE

POLISI waliostaafu na wengine wanaoendelea kuhudumu katika Idara ya Polisi, wamekilaumu Chama cha Ushirika cha Polisi (KPSS) na Chama cha Uwekezaji cha Utumishi (UIL) kwa kuwapunja fedha zao kwenye mradi waliowekeza na baadaye kuuzwa bila wanachama kufahamu.

Malalamishi hayo yametolewa na jumla ya polisi 16,000.

Kwenye stakabadhi ambazo Taifa Leo iliona, polisi hao wanadai kwamba walinunua shamba la ekari 20 karibu na mkahawa wa Safaripark mnamo 1989, kwa ahadi na matumaini kwamba wanachama wake wangefaidika.

Shamba hilo lilikuwa nambari LR8393.

Kwenye stakabadhi hizo, walisema polisi walilazimishwa kuwa wanachama wa chama hicho cha ushirika kupitia kamishna wa zamani wa polisi, marehemu Philip Kilonzo.

“Matumaini ya kila mwanachama yalikuwa ni kufaidika kutokana na ununuzi wa shamba hilo,” akasema Bw George Musamali, ambaye ni polisi aliyestaafu na mchanganuzi wa masuala ya usalama.

Anasema kuwa baada ya ununuzi wa shamba hilo, wanachama walijenga nyumba 31 , ambazo baadaye walizikodisha kwa Hoteli ya Safaripark.

“Baada ya ujenzi huo, kila mwanachama alikuwa akifaidika kutokana na kodi iliyokuwa ikilipwa na hoteli hiyo, japo kulingana na kiwango cha hisa zake,” akasema Bw Musamali.

Hata hivyo, alisema kuwa wanachama hawajui kuhusu vile usimamizi wa nyumba hizo ulibadilishwa kuwa chini ya kampuni ya Ruaraka Housing Estate Limited.

Anasema kuwa baadaye walifahamu kuwa shamba hilo limeuzwa na kile kimebaki ni chini ya ekari moja.

Malalamishi yao pia yanahusu ununuzi na uuzaji tata wa jumba la Utumishi House.

Kulingana na stakabadhi hizo, polisi walinunua jumba hilo kutoka kwa Chama cha Ushirika cha Matungulu, ambapo lengo lao lilikuwa ni kuwafaidi wanachama.

“Katika hali isiyoeleweka, jumba hilo liligeuzwa kuwa Chama cha Uwekezaji cha Utumishi. Kinaya ni kuwa, hilo lilifanywa bila ufahamu wowote wa wanachama. Pili, hawajakuwa wakipokea bonasi,”
akasema.

Kwa ushirikiano na maafisa walioathiriwa, Bw Musamali ametishia kwenda mahakamani akiwataka maafisa wa vyama hivyo viwili kueleza jinsi umiliki wa shamba na jumba hilo ulibadilishwa bila ufahamu wa wanachama.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Chama cha Uwekezaji cha Utumishi, Aloise Mbijiwe, alipuuzilia mbali madai hayo, akisema kuwa walalamishi wanafaa kuenda kwa maafisa wakuu wa Chama cha Ushirika cha Polisi Kenya kuuliza maswali hayo.

“Hao ni watu wanaotaka kujifaidi kwa kutumia njia za mkato. Wanafaa kuuliza maswali hayo kwa chama cha ushirika kwa polisi,” akasema Bw Mbijiwe, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Hata hivyo, Bw Musamali amesisitiza watafanya kila wawezalo kutafuta haki.