Polisi walia mishahara yao kupunguzwa

Polisi walia mishahara yao kupunguzwa

MARY WAMBUI na CHARLES WANYORO

MAAFISA wa polisi wapatao 1,000 wanapanga kushtaki Huduma za Polisi nchini na tume yake kulalamikia kupunguzwa kwa mishahara yao ya Novemba.

Maafisa hao ambao wamekuwa wakipata mishahara ya Daraja ya J sawia na Inspekta wa Polisi japo wangali katika kitengo cha Makonstebo waliofuzu elimu ya Chuo Kikuu walipigwa na butwaa walipopokea mishahara ya Daraja ya F, ambayo ni sawa na mishahara wanayolipwa makonstebo wa polisi.

Idadi kubwa ya maafisa wa polisi waliokuwa wametegemea mishahara yao kulipia mikopo mikubwa na kukatwa ada nyinginezo zinazohitajika, wameshindwa kukidhi mahitaji yao ya kimsingi kila mwezi kama vile kodi, chakula na masurufu.

Nakala za mishahara yao zinasoma mishahara ya kuanzia Sh53, Sh18 na hata Sh-7000 kwa baadhi yao.Nakala zilizoonwa na Taifa Leo kutoka kwa maafisa kote nchini zinaonyesha kuwa katika kiwango cha Daraja ya J, maafisa walikuwa wanapata kiasi cha Sh59,000 lakini mwezi huu walipokea Sh32,000.

Marupurupu yao ya makao yamepunguzwa kutoka Sh24,000 hadi Sh9,000 huku marupurupu ya kujisitiri (kwa polisi/walinzi wa magereza) yakipunguzwa kutoka Sh11,000 hadi Sh9,000.Hatua ya mishahara kupunguzwa inaathiri maafisa kutoka vitengo vyote ikiwemo DCI huku wengi wao wakiitaja kama shinikizo kwao wajihusishe na uhalifu ili kuongeza mapato yao.

Wanasema hatua hiyo huenda ikawakosesha ari ya kukabiliana na majukumu hatari hasa wakati huu ukanda huu unapokabiliwa na tishio la ugaidi. Afisa mmoja alieleza jinsi amekuwa akihudhuria mahojiano kadhaa ya kupandishwa cheo bila mafanikio licha ya kuwa na ujuzi wa kiwango cha juu.

“Mchakato wa kupandisha vyeo daima huwa na ubaguzi. Hatua ya kupunguza mishahara itaathiri shughuli za huduma za polisi nchini kwa sababu hatuwezi kujikimu na waliotusimamia kama wadhamini wataumia.”“Kuna tishio la ugaidi nchini na hatukutarajia kamwe kuwa tume hii itasababisha uhasama miongoni mwa maafisa,” ilisema taarifa hiyo.

Walilalamika kuwa hatua ya hivi majuzi ya kuwaajiri maafisa 300 wa jeshi haikuwa ya haki kwa sababu iliwafungia nje maelfu ya polisi waliofuzu vyuo vikuu ambao wamekuwa wakisubiri kupandishwa vyeo kwa miaka mingi.

“Inamaanisha walipunguza mishahara kuwalipa maafisa wapya wa jeshi? Alishangaa afisa wa kike akichelea kutajwa kwa kuhofia kusumbuliwa.Afisa mmoja miongoni mwa walioathiriwa alisema mabadiliko hayo yaliidhinishwa Jumanne iliyopita wakati kamati ilipokutana na kutekeleza Ijumaa wakati maandalizi ya mishahara ya Huduma za Polisi ilipokamilishwa.

Mamia ya maafisa walioshushwa vyeo wamekuwa wakijitahidi kuwasiliana na Naibu Rais William Ruto, Bw Raila Odinga na wanasiasa wengine wakitaka usaidizi wao. Wameandika barua inayosheheni vipengele tisa wakisema hatua hiyo itawavunja moyo maafisa, wengi wao ambao wanalipa mikopo na majukumu mengine ya kifedha.

NPS imekuwa ikijaribu kutekeleza amri iliyotolewa Machi 7, 2018 na aliyekuwa mwenyekiti wa NPSC wakati huo, Johnston Kavuludi, kwa lengo la kuwashusha hadhi maafisa waliopata vyeti vya digrii walipokuwa wakifanya kazi kama makonstebo.

Bw Kavuludi alisema baadhi ya maafisa waliingizwa kwenye orodha ya mishahara bila idhini ya Inspekta Jenerali wala Tume husika.

You can share this post!

TAHARIRI: Vyama vikubwa visitumie hila kuzuia uhamaji

Kivumbi 2022 marafiki wakipimana nguvu

T L