HabariSiasa

Polisi waliokubalia watu wenye corona kuingia Homa Bay watiwe adabu -Kaluma

April 20th, 2020 2 min read

Na VICTOR RABALLA na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma ameitaka serikali kuwachukulia hatua kali maafisa wa polisi wanaosimamia vizuizi vya barabara waliowaruhusu watu kusafiri kutoka Nairobi hadi kaunti ya Homa Bay.

Aliwataja maafisa hao kama wasiowajibika kwa kuwaruhusu watu kusafiri kutoka Nairobi hadi kaunti zingine ilhali serikali imezima safari hizo ili kuzuia kuenea kwa virusi kwa corona.

“Ikiwa watu wanaweza kuruhusiwa kusafiri kutoka Nairobi hadi Homa Bay hizi vizuizi vya barabara ni vya nini?” Bw Kaluma akauliza.

Alimtaka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuamuru kukamatwa kwa maafisa wote wa polisi waliokuwa katika vizuizi vya barabara wakati ambapo watu hao watu hao walipita.

“Maafisa hao pia wanafaa kuchunguzwa ikiwa wana virusi vya corona, watengwe kwa lazima na kisha wawasilishwe mahakamani kwa utepetevu kazini na kuvunja sheria za Afya ya Umma,” Bw Kaluma akaongeza.

Mbunge huyo alisema hayo baada ya dereva wa ambalansi moja iliyokuwa akisafirisha watu kutoka Nairobi waliojifanya kuwa wanaelekea Homa Bay kupatikana na virusi vya corona. Ambulansi hiyo ilibeba jeneza tupu.

Dereva huyo alipita vizuizi kadha vya polisi kabla ya maafisa wa polisi Homa Bay kufichua ujanga wao walipofunua jeneza hilo la kubaini halikuwa na maiti.

“Serikali inapasa kutangaza hatua ambazo imeweka kuhakikisha kuwa watu ambao wanaruhusiwa kusafiri kutoka Nairobi kwenda kaunti zingine wanachunguzwa ikiwa wana virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kusafiri,” akasema Bw Kaluma.

Alielezea hofu kwamba serikali hatua zozote zimechukuliwa na kuwasaka watu ambao walitangamana na wageni hao na kuwaweka katika karantini ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19 katika kaunti ya Homa Bay.

Bw Kaluma pia alimtaka Waziri Kagwe kufichua majina ya watu waliokuwa katika ambulansi hiyo, watu ambao aliwataka kama “wenye heshima kuu”.

“Ama kwa hakika serikali inafaa kufuatilia kwa maakini kaunti ya Homa Bay kwa sababu tayari wakazi wake wengi wameathirika pakubwa na magojwa mengine sugu huku ikikosa vituo vya afya visivyo na uwezo wa kukabiliana na magonjwa hatari kama vile Covid-19,” akaeleza.