Habari

Polisi wamtoa Sonko machozi mkutanoni

December 1st, 2020 2 min read

Na COLLINS OMULO

KIZAAZAA kilizuka jijini Nairobi jana Jumatatu polisi walipotumia gesi ya kutoa machozi kutawanya mkutano ambao Gavana wa Nairobi Mike Sonko na madiwani wanaomuunga mkono walikuwa wakiandaa kuhutubia wanahabari.

Bw Sonko alikamatwa na kuzuiliwa kwa muda kabla ya kuachiliwa huru huku madiwani hao wa vyama vya Jubilee na ODM, wakikimbilia usalama polisi walipowarushia gesi ya kutoa machozi.

Kisa hicho kilitokea katika boma moja eneo la Riverside mtaani Lavington, Nairobi.

Polisi walivamia boma hilo wakijihami kwa vitoa machozi, bunduki na rungu baada ya kudokezewa kuwa Bw Sonko na madiwani hao walikuwa wakiandaa mkutano na wanahabari kuelezea msimamo wao kuhusu hoja inayopangwa kumtimua ofisini.

Hali ya taharuki ilitanda madiwani hao walipokaidi amri ya polisi kuondoka katika boma hilo huku Bw Sonko akijaribu kuwarai polisi wasivunje mkutano huo.

Mambo yaliharibika zaidi maafisa hao walipowarushia madiwani gesi ya kutoa machozi na kuwafanya watawanyike kuokoa maisha yao.

Kwenye kizaazaa hicho, Bw Sonko alikamatwa na kusukumwa ndani ya gari la polisi. Baadaye aliachilia huru na kuondoka eneo hilo.

Kabla ya polisi kuvamia boma hilo, madiwani hao walioongozwa na diwani wa kuteuliwa Silvia Museiya, walisema hawaungi hoja ya kumtimua Bw Sonko ofisini wakiwalaumu wenzao kwa kughushi saini zao na kudai kwamba madiwani 86 walikuwa wameidhinisha atimuliwe.

Bi Museiya alidai saini hizo zilichukuliwa kutoka mkutano ambao madiwani walifanya awali. Alidai ni madiwani 17 pekee waliotia saini zao kuunga hoja hiyo.

“Madiwani hawakutia saini zao. Wale wachache waliotia saini walifanya hivyo baada ya kutishwa,” alisema.

Akafafanua: “Tuko hapa kusema kwamba tunamuunga Gavana Sonko na Idara ya Huduma ya Nairobi (NMS). Hatukatai NMS lakini tunachotaka ni heshima na utawala wa sheria. Tunasema bajeti ilikuwa na dosari ambazo zinafaa kurekebishwa ili wakazi wa Nairobi wapate huduma.”

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja alikashifu kukamatwa kwa Bw Sonko na kuwalaumu polisi kwa kutumiwa kuendeleza vita vya kisiasa.

“Kumkamata Bw Sonko kwa kukutana na madiwani wiki ambayo kuna mipango ya kumuondoa ofisini ni sawa na polisi kutumiwa kisiasa,” Bw Sakaja alisema kupitia ujumbe wa Twitter.