Habari Mseto

Polisi wanaoshukiwa kuiba hela ATM za Barclays kizimbani

May 2nd, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

WASHUKIWA watano wakiwemo maafisa wawili wa polisi na walinzi wawili wa kampuni ya G4S, Alhamisi walishtakiwa kwa wizi katika mitambo ya ATM ya benki ya Barclays jijini Nairobi.

Mabw Fredrick Herman Otiya, Daniel Orero Okindo, George Gachungu Njoroge na John Otieno Makambogo, walikanusha kwamba waliiba Sh2.8 milioni kutoka ATM za benki ya Barclays zilizopo Kenya Cinema Plaza, Moi Avenue, jijini Nairobi.

Ilidaiwa kwamba walitenda kosa hilo, wakishirikiana na watu wengine ambao hawakuwa kortini mnamo Aprili 16 mwaka huu.

“Mnamo Aprili 16, 2019 katika mtambo wa ATM wa benki ya Barclays ulioko Kenya Cinema Plaza, Moi Avenue jijini Nairobi, mlishirikiana na watu wengine ambao hawako mbele ya mahakama kuiba Sh2.4 milioni mali ya benki ya Barclays,” lilisema shtaka walilosomewa mbele ya Hakimu wa Milimani, Bw Kennedy Cheruiyot.

Katika shtaka la pili ilidaiwa kwamba walishirikiana kupanga njama za kutekeleza uhalifu ambao ni wizi wa pesa hizo. Mshtakiwa wa tano, Bw Patrick Nyoike Karanja, ambaye aliytajwa kuwa dereva wa teksi, alishtakiwa kwa kuiba Sh1 milioni.

Wote walikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu hadi Juni 5 kesi itakaposikizwa.