Habari Mseto

Polisi wanaowasaidia wezi wa mifugo wapokonywa silaha

April 10th, 2018 1 min read

Na MWANGI NDIRANGU

POLISI wa akiba katika baadhi ya sehemu za Kaunti ya Laikipia wamepokonywa silaha zao na serikali kwa kutuhumiwa kushirikiana na wahalifu kutekeleza wizi wa mifugo.

Kamishna wa kaunti hiyo Bw Onesmus Musyoki alithibitisha kwamba polisi 30 katika wadi ya Mukogodo Mashariki, katika Kaunti Ndogo ya Laikipia Kaskazini waliagizwa kurejesha silaha zao. Alisema kuwa watapigwa msasa kabla ya kukabidhiwa upya.

“Tumeagiza kamati ya usalama ya kaunti ndogo kuandaa upigaji msasa wa polisi wote wa akiba katika kata za Makurian, Ngwesi na Sieku. Wale ambao watapita zoezi hilo watarejeshewa silaha zao,” akasema Bw Musyoki.

Alikubali kwamba baadhi ya polisi hao waliajiriwa kwa haraka, akishikilia kuwa watazingatia tahadhari kubwa katika siku za baadaye ili kuepuka matumizi mabaya ya bunduki.

Kwa sasa, kuna jumla ya polisi 823 ambao wameajiriwa ili kuwasaidia polisi wa kawaida kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Polisi hao walinyang’anywa silaha hizo kufuatia wizi wa zaidi ya ng’ombe 800 katika shamba la Ole Naishu mwezi Januari mwaka huu.

Na hata baada ya operesheni kali kuongozwa na vikosi vya usalama kuwatafuta, ni wachache tu waliopatikana.

Kwa hayo, wakuu wa usalama waliwatuhumu polisi hao kushirikiana kisiri na wezi kutoka kaunti jirani ya Isiolo.

Lakini licha ya zoezi hilo, baadhi ya wakazi wa eneo la Mukogondo Mashariki wameeleza hofu kwamba huenda hilo likaongeza tishio la usalama.

Diwani wa wadi hiyo Daniel Nyausi alisema kwamba serikali ingetathmini njia zingine za kukabili hali hiyo, badala ya kuwanyang’anya bunduki.