Habari

Polisi wanasa muuzaji wa Heroin Lamu

May 1st, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

POLISI katika Kaunti ya Lamu Jumanne wamemkamata mwanamume wa miaka 42 baada ya kupatikana na sacheti 12 za Heroin na misokoto 7 mikubwa ya bangi.

Hassan Adam Hamisi (pichani) alikamatwa na polisi waliokuwa wakishika doria katika kivuko cha Mtangawanda, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, alisema pia walipata vijiko 20 pamoja na sinia, vifaa vinavyoaminika kutumiwa na mshukiwa ili kupima na kuuza Heroin eneo hilo.

Mshukiwa pia alipatikana na Sh4,990 pesa taslimu alizokuwa ameficha kwenye mfuko wake.

Alisema mshukiwa bado anazuiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi kabla ya kufikishwa kortini juma hili.

“Tumefaulu kumnasa mshukiwa wa ulanguzi na uuzaji wa heroni na bangi. Amekuwa akitafutwa na polisi kwa muda mrefu. Tumempata na sachet 12 za heroni ya thamani ya Sh 2,400 na misokoto mikubwa 7 ya bangi ya thamani ya Sh 3000.

Heroin, misokoto ya bangi, pesa taslimu na vijiko vya kupima alivyokamatwa navyo Hassan Hamisi Adam kaunti ya Lamu May 1, 2018. Picha/ Kalume Kazungu

Mshukiwa bado tunamzuilia kwa mahojiano zaidi kabla ya kumfikisha kortini wakati wowote kuanzia sasa,” akasema Bw Kioi.

Naye Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kitengo cha Jinai (CID) wa Kaunti ya Lamu, Paul Leting, alisema polisi wanafuata habari za ujasusi kuhusiana na mshukiwa huyo kwani anaaminika huenda anashirikiana na walanguzi wengine wakuu ili kuendeleza biashara ya kusambaza na kuuza dawa za kulevya kote Lamu.

Bw Leting aliwataka wakazi walio na habari kumhusu mshukiwa huyo na wengineo kujitokeza.

Aidha aliwataka wakazi hasa vijana kujiepusha na ulanguzi wa mihadarati.

“Vijana wengi hapa wanapotelea katika matumizi ya dawa za kulevya. Ningewasihi kujiepusha na mihadarati. Jamii pia iwe tayari kutoa ripoti kwa polisi ili kusaidia kukabiliana na janga hilo. Polisi wako macho ili kukomesha uozo huo Lamu,” akasema Bw Leting.