Habari

Polisi wanasa washukiwa wakichuuza noti za 1,000

June 16th, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

POLISI katika Kaunti ya Murang’a wanachunguza madai ya ulanguzi wa pesa, baada ya watu wawili kukamatwa kwa tuhuma za kukodisha pesa kwa wakazi na kuwataka walipe kwa kutumia sarafu mpya zilizozinduliwa majuzi.

Kamanda wa Polisi katika kaunti hiyo, Bw Josephat Kinyua, alisema washukiwa hao walikamatwa katika soko la Mukuyu baada ya wakazi kuwaarifu polisi kuwa walikuwa wakiwakodisha pesa kwa njia waliyotilia shaka.

Ili kukodishiwa fedha hizo, mtu alihitajika kuzirudisha kwa muda wa mwezi mmoja, lakini zikiwa kwa noti mpya. Mtu pia alihitajika kuwa na kitambulisho cha kitaifa pekee.

Afisa huyo alisema kuwa baada ya kukamatwa kwa watu hao, maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), walianza uchunguzi ili kubaini ukweli kuhusu shughuli za watu hao.

“Tunataka kuchunguza ukweli kuhusu madai ya wakazi, hasa katika wakati huu kuna noti mpya.

Huenda ikawa njama ya watu kujitajirisha kwa fedha walizopata kwa njia haramu kabla ya kukamilika kwa muda uliowekwa na Benki Kuu kubadilisha pesa za sasa,” alisema kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Hata hivyo, alisema kuwa wawili hao walisema walikuwa wakiwasajili wanachama wa chama kipya cha ushirika ambacho kitakuwa kikitoa mikopo midogo midogo kwa wakazi.

Alisema kuwa wawili hao wameagizwa kurejea kituoni wakiwa na stakabadhi zinazoonyesha uhalali wa chama hicho, huku uchunguzi ukiendelea.

“Tunataka kubaini ukweli kuhusu chama hicho, hali ambayo itatufanya kujua hatua ambayo tutachukua. Watu wanaweza kubuni njia za kulangua pesa, lakini tuko macho,” aliongeza.

Alisema kuwa wakazi waliwaarifu polisi kuwa washukiwa hao walianza biashara hiyo mnamo Alhamisi na ilishukiwa ni washirika wa baadhi ya wanasiasa.

Alisema kuwa walidai wametumwa na viongozi hao kuendesha biashara kwa niaba yao.