Polisi wanasa washukiwa wawili wa ujambazi

Polisi wanasa washukiwa wawili wa ujambazi

NA SAMMY KIMATU

MAKACHERO eneo la Makadara, Nairobi wamewakamata washukiwa wawili wa ujambazi wanaohusishwa na msururu wa wizi wakitumia bodaboda karibu na Airtel na BelleVue.

Mkuu wa polisi wa Makadara, Bw Timon Odingo alisema Fredrick Aura almaarufu ‘Sadam’ ambaye awali alitoroka baada ya kunyakua mkoba alipokuwa kwenye pikipiki karibu na makao makuu ya Airtel Kenya alikamatwa katika mtaa wa Villa, kaunti ndogo ya Embakasi Kusini.

Pikipiki ambayo mhalifu alitumia kutekeleza maovu. PICHA | SAMMY KIMATU

Katika eneo la South B, Gaddafi Okore, 32, alikamatwa kwa madai ya kuwaibia watu.

“Washukiwa hao ni miongoni mwa genge linaowatisha na kuwaibia watu hasa katika barabara ya Mombasa. Wanalenga kuiba simu, pesa na mikoba,” Bw Odingo alisema.

Baada ya kumkamata Gaddafi, polisi walipata kitambulisho cha taifa cha mlalamishi ambaye alikuwa ameripoti tukio hilo kwa polisi hapo awali.

Polisi walifanikiwa kupata nguo na simu ya rununu aina ya Samsung Core A3 mali ya mlalamishi.

Vilevile, Bw Odingo aliambia Taifa Leo kwamba ameshirikiana kumaliza genge hilo na Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Bw Felix Nyamai Kithuku kwa kuimarisha doria usiku na mchana.

“Tumeshirikiana na DCIO Felix Nyamai Kithuku kwa kuongeza maafisa zaidi wa polisi ambao waliovalia kiraia wakichanganyika na wengine waliovalia sare za polisi. Tunataka kuwaangamiza wahalifu hasa kati ya Uchumi na Airtel mkabala wa barabara ya Mombasa.

Bw Odingo aliwaomba wananchi kutoa habari kuhusu uhalifu ambazo huenda zikachangia kukamatwa kwa genge lililosalia.

“Wahalifu wanafanya kazi kwa kujipanga na wana kiongozi wao wa genge. Tuko kwenye rada na tuna maarifa, njia na mbinuzetu za kukabiliana na wahalifu hao. Siku zao zimehesabika,” Bw Odingo alionya.

Mmoja wa washukiwa waliokamatwa mnamo Desemba 06, 2022. Inadaiwa wao hupora pesa, simu na mikoba ya raia karibu na makao makuu ya Airtel Kenya, Mombasa Road jijini Nairobi. PICHA | SAMMY KIMATU

DCIO Kithuku aliambia wanahabari kwamba wawili hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Industrial Area ambapo wako chini ya ulinzi wa polisi na wanahojiwa.

Bw Kithuku aliongeza kuwa baada ya kupata taarifa thabiti kutoka kwa washukiwa, ndipo wakati mwafaka watakapowafikisha washukiwa hao mahakamani.

  • Tags

You can share this post!

Arati akana madai ya uhasama na Seneta Onyonka

Gavana Achani alalamikia MCAs kuchelewa kuidhinisha...

T L