Habari MsetoSiasa

Polisi wanatimua wakazi ardhini kiharamu – Jumwa

May 26th, 2019 1 min read

Na CHARLES LWANGA

MBUNGE wa Malindi Aisha Jumwa, amewalaumu polisi katika Kaunti ya Kilifi kwa kutumiwa kutekeleza amri ghushi za mahakama ili kuwafurusha wakazi kutoka mashamba wanakoishi.

Alidai kuwa maafisa wa polisi wamekuwa wakishawishiwa na mabwanyenye kwa kupewa pesa ili kufurusha wakazi mashambani mwao kupitia amri bandia za mahakama.

“Nimeziangalia amri hizi na kupata kuwa ni bandia lakini wakati maafisa wa polisi wanapewa pesa kidogo na mabwenyenye, wao huenda kufurusha wakazi ambao wameishi mashambani humo miaka na mikaka bila kujali,” alisema.

Mbunge huyo alikuwa akizungumza katika mkutano wa dharura wa kutatua mzozo wa shamba baada ya bwanyenye kuwasilisha amri ya kufurusha familia 600 katika shamba la ekari 30 eneo la Kingston huko Kwachocha.

Wakati huo huo, Bi Jumwa aliishutumu Tume ya Ardhi (NLC) kwa kupendelea matajiri katika jamii wakati wa kutatua kesi za dhuluma za mashamba na kukandamiza wakazi ambao ni masikini.

“Tume ya NLC haijatatua shida yoyote Malindi, Kaunti ya Kilifi na eneo la Pwani kwa jumla. Nina malalamishi ya kuwa Wamijikenda ambao wameishi shambani humo vizazi na vizazi hawapatiwi nafasi ya kujieleza na tume hiyo,” alisema.

Bi Jumwa alidai kuwa Tume ya NLC imekuwa ikitumikia mabwanyenye pekee yao na kudharau wakazi ambao ni maskini.

Bw Christopher Kambi ambaye ni mkazi wa Kwachocha ambapo pana mzozo wa shamba alisema eneo hilo limegeuzwa pahali pa malumbano kati ya polisi na wakazi.

Alisema kwamba huenda Kampuni ya Umeme Nchini (KP) ilishawishiwa kukata umeme eneo hilo kabla ya shughuli za kufurushwa kuanza asubuhi hiyo na mapema.

“Kesi ya mzozo wa shamba iko mahakamani na bado haijasikilizwa lakini bwanyenye amekuja na amri gushi akitaka kutufurusha,” alisema.