Habari Mseto

Polisi wanatumiwa kututishia – Wahadhiri

May 9th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Muungano wa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini (UASU) na Chama cha wafanyakazi wa vyuo hivyo (KUSU) wameshtumu serikali kwa kutumia polisi kuwashambulia na kuwanyanyasa wahadhiri wanaoshiriki mgomo.

Katibu Mkuu wa UASU Dkt Constantine Wasonga alisema kwamba dhuluma hizo katu hazitawalazimisha kusitisha mgomo huo na kuitaka serikali na manaibu chansela wa vyuo kutumia njia zinazokubalika ili kufikia makubaliano yatakayowarejesha madarasani

Baadhi ya vyuo vikuu alivyovitaja kwamba usimamizi wao umechukuliwa na Polisi ni Masinde Muliro, Maasai Mara, Pwani na Kenyatta.

“Tunalaani kwa kinywa kipana kuendelea kutumiwa kwa wakora na maafisa wa polisi katika vyuo vyetu ili kuwalazimisha wahadhiri kurejea darasani. Mgomo unaendelea wapende wasipende hadi watutatulie maslahi yetu,” akasema Dkt Wasonga.

Katibu huyo pia aliulaumu uongozi wa vyuo vyenyewe wakiwemo manaibu chansela kwa kutumia swala la mgomo kuzua uhasama mkubwa kati ya wahadhiri na wanafunzi. Katika siku za hivi karibuni wanafunzi wa baadhi ya vyuo wamekuwa wakiandamana na kupinga mgomo huo huku wakiwakabili wahadhiri wanaogoma.

“Serikali sasa imeamua kutugonganisha na wanafunzi ambao ni watoto wetu wakifikiria hilo litatutia uoga. Tunawaomba wanafunzi wasiende vyuoni kwa sababu wakora na polisi watawadhuru,” akasema

Aidha, katika onyo kali kwa serikali, kiongozi huyo alisema endapo mwanachama yeyote wa vyama hivyo viwili atajeruhiwa au kufariki kutokana na vitendo vya kihalifu vya polisi basi serikali iwe tayari kupokea lawama kubwa.

Kwa upande wake Dkt Charles Mukhwaya ambaye ni katibu mkuu wa chama cha KUSU alishangaa haja ya wao kuendelea kushirikishwa kwenye mikutano mingi na jopo lililoundwa na waziri wa elimu Amina Mohamed ilhali hawajawasilishiwa pendekezo mbadala la matakwa yao.

“Tunashinda katika vikao na jopo hilo ilhali wanachama wake hawajawahi kutupa pendekezo lao lakini wanatarajia mgomo usitishwe. Dhuluma wanazotenda dhidi ya wahadhiri ndizo zinazidi kutonesha vidonda vyetu,” akasema Dkt Mukhwaya

Wawili hao walikuwa wakizungumza katika mkutano na wanahabari katika makao makuu chama katika Jumba la Unafric mjini Nairobi.