Polisi waonya wanafunzi wanaochoma shule kuwa watafungwa kama wahalifu wengine

Polisi waonya wanafunzi wanaochoma shule kuwa watafungwa kama wahalifu wengine

Na ALEX KALAMA

Kamanda wa polisi wa Kaloleni, Kaunti ya Kilifi, Bw Ezekiel Chipukoeny amewaonya wanafunzi wanaosababisha uharibifu wa mali shuleni kwamba watakabiliwa kisheria.

Afisa huyo wa usalama alisisitiza kuwa serikali haitaruhusu ama haitasaza mtu yeyote anayetekeleza uhalifu licha ya umri au nafasi yake katika jamii.Akizungumza na wanahabari huko Kaloleni, Bw Chipukoeny alisema idara ya upelelezi katika eneo bunge hilo inaendelea kuchunguza visa vya utovu wa nidhamu vilivyopelekea uharibifu wa mali katika shule ya upili ya St.George’s na ile ya Ngala Memorial.

‘Kuchoma ni uhalifu, kwa hivyo kwa wale ambao watapatikana walihusika kabisa na hayo mambo ya kuchoma, tutawakamata na tutawapeleka kortini. Kulingana na Katiba mtu akifanya makosa, sheria inachukua mkondo wake.

Kwa hivyo haijui kama ni mtoto ama ni mtu mzima,’ alisema Bw Chipukoeny.Hata hivyo afisa huyo wa polisi amewataka wazazi kuwajibika na kuhakikisha wanafuatilia mienendo ya watoto wao. ‘Ukisikiza ile sababu wanasema, hakuna hata sababu,kwa hivyo tuachie wale ambao wanachunguza watajua wale ambao walihusika.

Na wazazi tafadhalini kila wakati tuangalie watoto wetu na tuwachunguze tabia zao ukiona mtoto anaanza kuwa na tabia ambazo siza kawaida ni vizuri mzazi uongee na mtoto wako,’ alisema Bw Chipukoeny.

Wakati huo huo Bw Chipukoeny alisisitiza haja ya wazazi kufanya kazi kwa ukaribu mno na uongozi wa shule hasa zile za upili akisema hatua hiyo itaimarisha sekta ya elimu na nidhamu katika shule zote kaunti hiyo..

You can share this post!

EACC yaambia Waiguru ‘tuliza boli’

Ofisi za Arati zazua mzozo baina ya wafuasi wa ODM

T L