Habari Mseto

Polisi wapata sukari 'hatari', wakamata mshukiwa

August 17th, 2019 2 min read

Na WINNIE ATIENO

MAAFISA wa polisi 15 kutoka vitengo tofauti tofauti wamepata sukari ‘hatari’ katika mtaa wa mabanda wa Bangladesh, Mombasa iliyokuwa imeibwa kutoka katika ghala la Bollore huko Changamwe, wiki iliyopita.

Wakazi wa mtaa huo ambao huwa hawaogopi kuzungumza kwenye kamera hata hivyo wameshindwa la kusema Jumamosi baada ya maafisa wa polisi kugundua sukari hiyo inayoshukiwa kuwa na ‘sumu’ ilikuwa imefichwa katika mtaa huo wa mabanda.

Mshukiwa wa kike ambaye anajulikana sana mtaani humo, alishikwa na maafisa wa polisi baada ya sukari na zaidi ya magunia 800 ya mbolea kupatikana kwenye maskani yanayoaminika kuwa yake.

Wakuu wa usalama katika Kaunti ya Mombasa wamekataa kuzungumzia suala hilo, huku wale waliokuwa wakiendeleza operesheni hiyo vilevile wakifanya mambo yao kimyakimya.

“Hili suala ni kubwa sana; acha wakubwa ambao wako makao makuu watalizungumzia. Hapa tunafanya uchunguzi tu,” amesema mmoja wa wapelelezi.

Mkazi mmoja wa kiume ameelezea hofu yake.

“Kama polisi wamekataa kuongea mimi ni nani nijifanye kimbelembele halafu nikajipata pabaya? Mwenye mali ni mtu ambaye anajulikana na watu wengi sana. Nina watoto wadogo na siwezi kulizungumzia suala hili; sitaki kufa mapema,” amesema mwanamume huyo.

Kulingana na wapelelezi, bidhaa hiyo ilifichwa kwenye magunia ya mbolea ya kilogramu 50.

“Tumekesha hapa kuanzia Ijumaa usiku tukilinda mali hii,” amesema afisa mwingine.

Taharuki

Taharuki imetanda eneo hilo huku magari ya maafisa wa upelelezi yakimiminika hapo.

Mshukiwa ameingizwa kwenye gari la polisi akiendelea kuhojiwa huku baadhi ya mifuko ya mbolea hiyo ikipakuliwa kwenye lori la polisi.

“Huyu mama anaogopewa na anajulikana na maafisa wa polisi. Kama ni sukari ya sumu, je wakazi wameuziwa? Kuna hatari kubwa sana hii nchi,” amesema mkazi mmoja, Bw Juma Omolo.

Hata hivyo, afisa mkuu wa upelelezi wa Mombasa Urban, Bw Anthony Muriithi amewataka Wakenya wawe na subira wakati uchunguzi unaendelea.

“Tumepata mbolea, tunaendelea kuchunguza suala la sukari, kwa sasa jambo liloko ni tuwe na subira,” amesema Bw Muriithi.

Kulingana na afisa mwingine ni kwamba sukari hiyo na mbolea ilikuwa imefichwa kwenye vyumba vinne vya mshukiwa huyo.