HabariSiasa

Huenda watumishi wa Ruto wakatupwa jela kwa wizi wa mayai

April 30th, 2019 1 min read

Na WYCLIFFE KIPSANG

WAFANYIKAZI nyumbani kwa Naibu Rais William Ruto eneo la Sugoi huenda wakafungwa jela kuhusiana na wizi wa kreti kumi za mayai.

Mkuu wa Polisi wa Eldoret Magharibi, Bw Zachariah Bittok, alisema maafisa wake wanawachunguza wafanyikazi wanne katika makazi ya Naibu Rais, baada ya meneja wa shamba hilo kuripoti kuibwa kwa trei 10 ambazo huwa na mayai 360 kwa njia ya kutatanisha.

 

“Uchunguzi wetu wa mwanzo ulifichua kwamba wafanyakazi wanne wanaoishi karibu na makazi ya Naibu Rais walihusika na wizi huo lakini wote walikanusha. Polisi baadaye waliendesha uchunguzi wao na trei zenye mayai hayo zikapatikana. Washukiwa walinaswa na kreti mbili, tatu na zaidi na tunaendelea kuwahoji,” akasema Bw Bittok.

Kando na kuwekeza katika miradi mingine ya kilimo, Naibu Rais anashiriki kilimo cha ufugaji wa kuku katika shamba lake la Sugoi ambalo linapatikana kilomita chache tu kutoka mji wa Eldoret.

Dkt Ruto ambaye alikuwa na mikutano kadhaa ya kisiasa katika eneo la Bonde la Ufa, hakuwa nyumbani wakati wizi huo ulipotokea.

Mnamo Jumamosi, Naibu Rais alihudhuria mazishi ya mwanawe Rais Mstaafu Daniel Moi, Jonathan Moi katika kijiji cha Kabimoi, eneobunge la Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo. Siku iliyofuatia alihudhuria ibada ya maombi eneo la Molo akiwa ameandamana na Gavana wa zamani wa Kiambu William Kabogo.

Katika kisa kingine tofauti na hicho, makazi hayo ya Naibu Rais yalivamiwa mnamo Julai 2017 na wahalifu, uvamizi uliodumu kwa siku nzima.

Hata hivyo, haijaeleweka hadi leo jinsi wavamizi hao wanaodaiwa kujihami vikali walifaulu kuwashinda askari langoni na kuingia kwenye makazi hayo ambayo hulindwa vikali kutokana na hadhi ya Dkt Ruto nchini.

Kabla ya kutokea kwa uvamizi huo wa saa tano asubuhi, Dkt Ruto alikuwa nyumbani na akatoka kuenda kuungana na Rais Uhuru Kenyatta kwa mkutano wa kisiasa mjini Kitale katika kaunti jiarani ya Trans Nzoia.