Polisi wapewa idhini ya kupiga risasi na kuua wahalifu wa magenge hatari

Polisi wapewa idhini ya kupiga risasi na kuua wahalifu wa magenge hatari

NA WINNIE ATIENO

MAAFISA wa polisi wamepewa idhini ya kuwapiga risasi na kuwaua magenge ya vijana wanaoendelea kuhangaisha wakazi na watalii kaunti ya Mombasa.

Wakuu wa usalama eneo la Pwani walisema magenge yatakapopatikana wakijihusisha na uhalifu watapigwa risasi papo hapo.

Kikosi maalum kitatumwa Mombasa kukabiliana na vijana hao washukiwa wa ujambazi wanaotumia silaha butu kuvamia wakazi na kuwaibia.

Kuna zaidi ya makundi 10 ya uhalifu wakiwemo vijana walioacha shule na kujiunga na Wajukuu wa Bibi, Wakali Wao, Wakali Kwanza, Wakware Babies, Watalia, Mawayo, Temeke na Chafu ambao wanaendelea kuwahangaisha wakazi Mombasa, wafanyabiashara na watalii.

Himaya ya makundi hayo ambao wanatumia dawa za kulevya ni Old Town, Likoni na Kisauni.

Hivi majuzi walinaswa kwenye kamera ya CCTV wakivamia wakazi hasa maeneo ya Old Town na kuwaibia.

Kikosi hicho maalum kitaanza msako rasmi wiki ijayo ili kuhakikisha makundi hayo ya uhalifu yanaangamizwa ili wasitumike kuzua ghasia wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

“Mombasa inafaa kuwa salama na wakazi waishi kwa amani. Lazima tukomeshe ghasia zozote. Kikosi maalum kitafika Mombasa na tutashirikiana kuangamiza magenge hayo. Wazazi kuweni makini na watoto wenu tushawaonya. Tutasafisha mji kabla uchaguzi mkuu. Yeyote atakayekamatwa akiiba atashtakiwa kwa kosa la wizi wa mabavu na hatma yake ni kifo,” alionya kamanda wa polisi wa Pwani Bw Titus Karuri.

Kwenye kikao maalum cha usalama huko Kisauni, Bw Karuri alisema kuchipuka kwa makundi hayo ni hatari kwa usalama, hata hivyo alisema kikosi maalum kitakachotumwa Mombasa kitakabiliana nao.

Alisema washukiwa 70 wamekamatwa tangu msako dhidi yao kuanza.

“Polisi akikukamata ukiiba sheria inamruhusu kukupiga risasi na kukuua bila kukuonya. Tuko na risasi za kutosha kutekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa sheria,” alionya Bi Karuri.

Mshirikishi wa eneo la Pwani Bw John Elungata alionya vijana wa Mombasa dhidi ya kujihusisha na uhalifu.

“Magenge huchipuka wakati wa uchaguzi mkuu ili kuzua ghasia na kusimamisha au kuhujumu zoezi la uchaguzi. Lakini tuko wima kukabiliana na majangili, tunawaonya wanasiasa dhidi ya kushirikiana na wahalifu,” alisema Bw Elungata.

Wazee wa mitaa na wakazi waliombwa kushirikiana na maafisa wa polisi kisafisha mji huo dhidi ya magenge ya ujambazi.

“Tutawachukulia hatua kali za kisheria wanasiasa wanaoendelea kuwafadhili magenge ya majambazi. Hulka hii huchipuka wakati wa uchaguzi,” alisema Bw Elungata.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Mrithi wa Uhuru aendeleze uhuru wa kujieleza...

Juventus pazuri kuipiku PSG, Real kunasa Pogba

T L