Polisi wapigana mmoja akimlaumu mwingine kwa kujisaidia mlangoni

Polisi wapigana mmoja akimlaumu mwingine kwa kujisaidia mlangoni

Na BRIAN OJAMAA

MAAFISA wawili wa polisi wanaohudumu katika eneo la Cheptais, eneobunge la Mlima Elgon, Bungoma, huenda wakachulikiwa hatua za kinidhamu baada ya kupigana hadharani Jumapili asubuhi, mmoja akimlaumu mwenzake kwa kulewa na kukojoa kwenye mlango wa nyumba yake.

Afisa wa cheo cha juu Paul Gitangita ambaye anasimamia kituo kidogo cha polisi Kopsiro, alipigana na afisa wa cheo cha konstebo, Daniel Sembe kutokana na kile kinachodaiwa kuwa mgogoro wa muda mrefu.

Lau sio raia waliokuwa karibu kufika na kuwatenganisha, mapigano hayo yangewasababishia majeraha mabaya.

Maafisa hao wawili baadaye walielekea katika kituo cha polisi na kuandikisha taarifa kila mmoja akimlaumu mwenziwe.

Bw Gitangita alikuwa wa kwanza kupiga ripoti kuwa Bw Sembe na mkewe Rose Onyango walimvamia kwa mawe na silaha butu.

Alidai wawili hao walichangia majeraha aliyoyapata kichwani.Kwa upande mwingine, Bw Sembe naye aliandikisha taarifa akisema Bw Gitangita alimfanya apate majeraha mabaya katika mguu wake wa kushoto kwa kutumia silaha butu.

Akithibitisha kupokea malalamishi ya polisi hao wawili, OCPD wa Cheptais Benjamin Wambua alisema, suala hilo linatatuliwa na vitengo husika ndani ya idara hiyo.

Bw Wambua alifichua kuwa afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha Kapkatenya, Abdoo Kiptoo alitembelea mahali ambapo polisi hao walipigana na akaafikiana nao kuwa tukio hilo litatuliwe na afisa wa cheo cha juu kituoni humo.

Bw Wambua alisema kuwa Bw Sembe alikuwa na mazoea ya kukojoa kwenye mlango wa mwenzake kila alipokuwa ameelewa na kusababisha mapigano hayo.

“Wawili hao hugombana kila mara wakiwa wamelewa. Wananchi na Naibu Chifu David Taboi walifika na kuwatenganisha,” akasema.

Polisi hao walikuwa na majeraha mabaya na wakakimbizwa katika zahanati ya Kapsambu walikotibiwa kisha wakaruhusiwa waende nyumbani.

Alisema bado usimamizi wa kituo hicho cha polisi haujafanya maamuzi ni adhabu ipi ya mwanzo wawili hao watapewa uchunguzi ukiendelea.

Bw Wambua alisisitiza kuwa maafisa wote lazima wazingatie maadili ya kazi na mgogoro unapotokea basi lazima wausuluhishe kwa ustaarabu unaohitajika.

“Kama wao ndio wanaonyesha sifa mbaya, basi raia watawaiga kivipi? Wanafaa wazingatie maadili ya utendakazi badala ya kupigana hadharani kuhusu mambo yanayoweza kutatuliwa kwa urahisi,” akasema.

Mkazi wa Cheptais Derrick Kirwa, alisema polisi hao walikuwa wakiishi katika makazi mabovu ambayo hayana hata vyoo huku akitaka serikali iwajengee nyumba mpya.

You can share this post!

Utata zaidi kuhusu mustakabali wa Messi kitaaluma Barcelona...

Wanatenisi wa Kenya waanza mazoezi ya uwanjani baada ya...