Habari

Polisi wapoteza mamilioni ya wizi

September 25th, 2019 2 min read

Na BRIAN OCHARO

KUNDI la maafisa wa polisi limo mashakani baada ya kukosa kuwasilisha mahakamani Sh25.9 millioni ambazo zilikuwa sehemu ya zaidi ya Sh300 milioni zilizoibiwa kutoka kwa kampuni ya G4S mjini Mombasa miaka tisa iliyopita.

Kampuni hiyo ilikuwa ikisafirisha Sh313 milioni kutoka Mombasa hadi Nairobi wakati ziliibiwa, ikidaiwa wafanyakazi wa kampuni hiyo walipanga njama hiyo ya wizi.

Karatasi zilizowalishwa mahakamani zaonyesha polisi walipata pesa hizo kutoka kwa washukiwa lakini hawakuziwasilisha mahakamani kama ushahidi wakati watu wanane walishtakiwa.

Haya yaliwekwa wazi wakati Jacob Mutuku Musau, Sylvester Mbuli Mbuvi na Amos Mutuku Musyoka walifika katika mahakama hiyo kudai fedha hizo ambazo walisema kuwa, zilikuwa zao za biashara na walitaka warudishiwe kuendeleza biashara zao.

Watatu hao walimwambia Hakimu Mkuu Edna Nyaloti kwamba, hawakupatikana na hatia katika kesi hiyo baada ya kukamatwa miaka tisa iliyopita.

Kupitia kwa wakili wao Leonard Mbuvi, watatu hao waliambia mahakama kuwa, fedha hizo hazikuwa sehemu ya zile ambazo ziliibiwa kampuni ya G4S, bali zilikuwa zao za kufanyia biashara.

“Tumejaribu njia zote polisi waturudishie hizo pesa lakini wamekataa licha ya kuwa wanazihifadhi pesa hizo na bidhaa zingine za nyumbani ambazo walichukua katika makazi yetu,” watatu hao walisema.

Watu hao sasa wanataka afisa aliyekuwa akichunguza kesi hiyo, Bw Paul Chebet akamatwe na kufikishwa mahakamani ili kuelezea mahali zilipo fedha hizo.

Mahakama hiyo iliaambiwa kuwa, Bw Chebet amekuwa akidinda kufika mahakamani licha ya kupewa barua za kutaka afike kortini kujibu maswali kuhusu fedha hizo.

Afisa Mkuu wa Upelezi wa Jinai Anthony Mureithi alifika mahakamani na kusema kuwa, ni Bw Chebet anayeweza kuelezea zilipo fedha hizo kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa mchunguzi wa kesi hiyo.

Bi Nyaloti hata hivyo alikataa kutoa amri Bw Chebet akamatwe akisema kuwa, fedha hizo hazikuwasilishwa kortini hivyo basi mahakama yake haina mamlaka ya kutoa amri hiyo.

Hakimu huyo aliwauliza watatu hao watafute njia nyingine ya kufuatilia fedha hizo kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti au kwa kushtaki idara polisi.

Watatu hao ni miongoni mwa washukiwa watano ambao walishukiwa kuhusika katika wizi wa fedha hizo uliotekelezwa Februari 12, 2010.

Walishtakiwa pamoja na wafanyikazi wawili wa kampuni ya G4S Bw Sylvester Mbisi Mutua na Bw Humphrey Wekesa Wanjala.

Wengine ambao walikabiliwa na mashtaka hayo ni Bi Eunice Mwende Musyoka, Bw Francis Kitonyo, Bw Humphrey Kabanga Njau na Bw Patrick Karanja Njau, ambao waliachiliwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi dhidi yao.

Hata hivyo, Bw Mutua na Bw Wanjala walihukumiwa kifungo cha miaka kumi kila mmoja gerezani mnamo 2017 baada ya kupatikana na hat iya ya wizi wa mali hizo, ambazo zilikuwa zinasafirishwa na mwajiri wao.

Inasemekana kiwango kidogo sana ya Sh313milioni ambazo ziliibwa zilipatikana huku zaidi ya Sh200milioni zikipotea kabisa.