Polisi warai wananchi wasitoroke maeneo waliyojisajili kwa kura

Polisi warai wananchi wasitoroke maeneo waliyojisajili kwa kura

WINNIE ATIENO NA KNA

MAAFISA wa usalama wameomba wananchi wasihame maeneo ambapo walijiandikisha kupiga kura, na kuahidi kuwalinda.

Wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Pwani, Bw Titus Karuri, walisema idara ya usalama imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha uchaguzi utafanywa hadi kukamilika kwa amani.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Bw Ronald Mwiwawi, alisema siku ya uchaguzi inafaa kuwa kama nyingine yoyote na hivyo kusiwe na wasiwasi.

“Kama watu wanasafiri, acha iwe ni kwa sababu wanaenda kupiga kura wala sio kwa sababu wanatoroka kwa uvumi kuhusu ghasia,” akasema Bw Mwiwawi.

Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini, Askofu Mkuu Martin Kivuva, alisema ingawa wananchi wana haki ya kuhamia kwingine iwapo wanahisi hawako salama, itakuwa vyema kama watapata nafasi ya kutekeleza wajibu wao wa kujichagulia viongozi.

Alieleza kuwa, kuna wanasiasa ambao hutumia taharuki kuzuia wananchi wasipige kura, na hivyo nchi huishia kuwa na viongozi wasiofaa.

“Tunatumai hakuna watu ambao wanajipanga kuanza fujo popote pale. Wanasiasa watulie wangoje tupige kura tuone matokeo. Tusiogope. Kuweni na ujasiri mjiandae kupiga kura,” akasema.

Bw Hussein Adan kutoka kwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) eneo la Pwani, alisema watafuatilia mienendo yote ya polisi ili kuepusha visa vya dhuluma dhidi ya raia na vilevile, dhuluma dhidi ya polisi.

  • Tags

You can share this post!

Wakiuka sheria kwa kupeleka siasa kanisani

Wavuvi Lamu sasa kushiriki uchaguzi

T L