Habari Mseto

Polisi warudisha Kenya enzi za giza

January 13th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

CHAMA cha Wanahabari (KUJ) kinataka hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa wa polisi waliomshambulia mpiga picha wa gazeti la Taifa Leo, Laban Walloga akiwa kazini.

Katibu mkuu Bw Erick Oduor, Jumatatu alitishia kuripoti serikali kwa Umoja wa Mataifa (UN) kwa kukosa kulinda uhuru wa wanahabari.

“Wiki moja iliyopita wanahabari watatu walidhulumiwa na polisi. Hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya maafisa hao licha yao kupiga ripoti,” akasema Bw Oduor.

Bw Walloga alikuwa akipiga picha katika maandamano ya kupinga hatua serikali kulazimisha usafirishaji wa mizigo kwa treni ya SGR pekee.

Maandamano hayo yamekuwa yakifanyika jijini Mombasa kila siku ya Jumatatu, ambapo wakazi wanadai hatua hiyo imedidimiza uchumi wa eneo hilo ambalo rasilimali yake kuu ni bandari.

Mpiga picha huyo alieleza jinsi mmoja wa maafisa wa polisi kwenye maandamano hayo alivyompiga kwa rungu bila sababu.

Picha zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha afisa huyo akimrushia rungu Bw Walloga, aliyejaribu kutoroka.

“Nilikuwa kazini na hata nilimuonyesha kitambulisho cha kazi na kamera yangu. Hakutaka kunisikiza. Alinifukuza. Alijaribu kunigonga kwa mkebe wa vitoa machozi lakini nikahepa. Baadaye alinigonga kwa rungu,” akasema.

Wengine waliohangaishwa na kukamatwa wakati wa maandamano hayo ni diwani wa wadi ya Jomvu Kuu, Bw Shebe Mukonoo, na maafisa wa shirika la Haki Afrika wakiwemo Bw Hussein Khalid na Mathias Shipeta.

Jana haikuwa mara ya kwanza kwa mpiga picha huyo kushambuliwa na maafisa wa polisi akiwa kazini.

Mnamo Agosti 2018, Bw Walloga alikamatwa pamoja na mpiga picha wa runinga ya NTV, Bw Karim Rajan walipokuwa wanapiga picha hoteli moja kwenye ufuo wa Bahari Hindi ambayo imekiuka kanuni za mazingira.

Matukio ya wanahabari kunyanyaswa na maafisa wa polisi nchini si jambo la jipya licha ya washikadau mbali mbali kuendelea kupigania uhuru wa uanahabari.