Habari Mseto

Polisi wasaka mlanguzi anayelazimu watu kuvuta bangi yake

January 9th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

POLISI katika Kaunti ya Murang’a wanamsaka mshukiwa wa ulanguzi wa bangi anayedaiwa kuwalazimu wanaotoa habari kumhusu kuvuta bangi.

Kwa mujibu wa mshirikishi wa mpango wa Nyumba Kumi eneo la Kigumo, Bw James Karanja, mwanamume huyo akishuku kuwa umetoa habari kwa maafisa wa usalama huwa anakunyemelea na kukulazimisha uvute bangi.

Bw Karanja alieleza jinsi mwanamke wa miaka 28, ambaye alidaiwa kuwa jasusi wa polisi, alivyolazimishwa kuvuta bangi mkesha wa mwaka mpya hadi akazirai.

“Pia, kuna mzee mmoja wa miaka 68 ambaye mlanguzi huyu alimlaumu kuwa huwa na mazoea ya kumwambia akome kuuza bangi. Alimtandika kisha akamshurutisha avute msokoto mzima wa bangi. Kwa siku tatu mzee huyo alionekana kurukwa na akili. Ilitubidi tumpe maziwa lita mbili kwa siku ndipo apate nafuu,” akasema Bw Karanja.

Polisi wamemtambua mwanamume huyo kama Muchiri Wambui kutoka kijiji cha Kabaria, Kaunti Ndogo ya Kigumo.

Mwaka 2019,  mwanamume huyo aliripotiwa kumshurutisha nyanya wa miaka 80 kuvuta bangi alipolalamika kuhusu waraibu kutumia shamba lake kuvuta bangi.

Kwa mujibu wa kamishna wa Kaunti ya Murang’a, Mohammed Barre, polisi waliarifiwa kuhusu mwanamume huyo na anasakwa.

Bw Karanja alionyesha Taifa Leo jumbe zilizotumwa na wananchi kwa Bw Barre, ambazo zinahusisha maafisa wa utawala eneo hilo wakiwemo machifu na maafisa wa polisi wanaodaiwa kumkinga mlanguzi huyo.

Wateja wa mlanguzi huyo wameripotiwa kuwa watoto wa shule za upili na msingi, taasisi za kiufundi na vijana wengine.

Chifu wa wadi ya Muthithi, David Kamau allisema kuwa amehusika katika kumsaka mlanguzi huyo.