Polisi wasaka mshukiwa wa ugaidi aliyekwepa mtego wao

Polisi wasaka mshukiwa wa ugaidi aliyekwepa mtego wao

SIAGO CECE na FARHIYA HUSSEIN

MAAFISA wa polisi wanamtafuta mshukiwa wa ugaidi anayeaminika alikwepa mtego wao Jumatatu, wakati walipokamata wengine wawili katika kivukio cha feri Likoni, Kaunti ya Mombasa.

Duru zimefichua kuwa, kulikuwa na mpango wa kutekeleza shambulio katika maeneo tofauti Mombasa mnamo Agosti 27, 2021 kuadhimisha siku ambapo Sheikh Aboud Rogo aliuawa baada ya kuhusishwa na itikadi kali ikidaiwa zinazochochea ugaidi.

Washukiwa wawili waliokamatwa hawakufikishwa mahakamani Jumanne jinsi ilivyotarajiwa, polisi wakisema wanataka kuomba waendelee kukaa kizuizini kwa muda ambao watakuwa wanaendeleza msako kutafuta wenzao.

Mshukiwa mmoja aliyekamatwa ni raia wa Kenya na mwenzake ni wa Tanzania, wana umri kati ya miaka 30 na 35, na wote walikuwa wamerudishwa nchini baada ya kukubali kuasi kikundi cha magaidi cha al-Shabaab.

Imefichuka kuwa, msako umepangiwa kufanywa katika mitaa ya Mombasa inayoaminika kuwa maficho ya washukiwa wa ugaidi na wasaidizi wao.

Mshukiwa wa tatu anayetafutwa amesemekana alikuwa amebaki Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale, wakati wenzake wawili walipokuwa wakielekea Mombasa wakiwa na silaha kama vile bunduki na vifaa vya kutengeneza mabomu.

Salim Rashid Mohammed almaarufu kama Chotara, 28, amedaiwa aliwahi kuhusika katika kikundi cha kigaidi cha ISIS, na kupanga mashambulio mbalimbali maeneo ya Kusini mwa Pwani.

Video ambazo hatungeweza kuthibitisha uhalisia wao, zilimwonyesha akikata shingo ya mtu ambaye hakutambulika, na baadaye akamwamuru mvulana mdogo wa takriban umri wa miaka minane pia afanyie mwingine hivyo.

Afisa wa ngazi za juu katika idara ya polisi aliambia Taifa Leo kwamba mshukiwa huyo amethibitishwa alirudi nchini majuzi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kupitia Tanzania.

Alikuwa amekamatwa katika mwaka wa 2016 lakini akaachiliwa kwa dhamana baada ya ushahidi wa kuendeleza kesi kukosekana.

Habari za kijasusi zilionyesha kuwa ni mshirika wa karibu wa mfanyabiashara Abdulhakim Salim Sagar, ambaye alikamatwa na polisi wa kupambana na ugaidi hivi majuzi.

Bw Sagar alidaiwa kufadhili shughuli za kigaidi, na ni shemejiye marehemu Sheikh Aboud Rogo.

Katika tukio la Jumatatu, polisi walipata bunduki mbili aina ya AK-47, vifaa vya kutengeneza mabomu, panga na aina nyingine za silaha katika gari aina ya Probox ambalo washukiwa wawili walikuwa wakisafiria.

Kando na hayo, polisi pia walipata ramani za vituo vya polisi vya Makupa na Central, na karatasi zilizokuwa na maelezo kuhusu duka kuu la Naivas Nyali na Kanisa la Jesus Celebration Centre (JCC), ikiwemo kuhusu aina ya usalama ulioekwa katika sehemu hizo.

“Inavyoonekana, walitaka kutambua sehemu ambayo ni rahisi kushambulia. Walikuwa wanakuja Mombasa kushirikiana na wenzao,” duru zikaambia Taifa Leo.

Akithibitisha tukio hilo, Mshirikishi wa Eneo la Pwani, Bw John Elungata, alisema mmoja wa washukiwa hao alikuwa akiishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na akawasiliana na wenzake walio nchini kuhusu mipango ya shambulio hilo.

“Polisi sasa wanawatafuta wenzake ambao wanaaminika wako Mombasa. Uchunguzi bado unaendelea ili kubainisha habari zaidi kuhusu mipango ya shambulio,” akasema.

You can share this post!

Uhuru asimamisha jaji kazi

Pasta mfuska anusurika kichapo