Polisi wasaka ngariba kwa kuwakeketa wanawake

Polisi wasaka ngariba kwa kuwakeketa wanawake

Na OSCAR KAKAI

MAAFISA wa polisi katika kaunti ndogo ya Kacheliba, Kaunti ya Pokot Magharibi, wanamsaka mwanamke anayedaiwa kuwakeketa wanawake watano na wasichana wawili, katika Lokesheni ya Emboasis, juma lililopita.

Afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha Kacheliba (OCS), Bw Tom Nyang’au, alisema kuwa maafisa wa polisi wamepiga kambi katika boma la mama huyo kwa siku mbili, lakini wanashuku kuwa ametorokea nchi jirani ya Uganda baada ya kupashwa habari kuwa anasakwa.

Bw Nyang’au alisema kuwa mama huyo, alivuka mpaka baada ya kuwakeketa wanawake hao na walipofika alikofanyia kitendo hicho, wanawake walikuwa wamepata afueni na hawakuwapata.“Kati ya tarehe 11 na 16 Oktoba, akina mama watano na wasichana wawili, walikeketwa na tulifaulu kuwakamata waume wa wanawake wawili na mama wa wasichana hao wawili,” alisema.

Aliongeza kuwa bado wanawatafuta waliomsaidia mama huyo kuwakeketa wasichana na akina mama hao.Pia alisema kuwa kwenye lokesheni hiyo, kuna akina mama watatu ambao hufanya kazi ya ukeketaji na maafisa wa polisi walifaulu kuwakamata wawili ambao wanazuiliwa.

Ukeketaji wa wasichana ni marufuku nchini Kenya hata ingawaje baadhi ya jamii zingali zinauendesha kisiri.Serikali na mashirika tofauti imekuwa ikiendeleza mipango ya kukomesha desturi hiyo ambayo imebainishwa kuathiri maisha ya wasichana na pia afya yao pamoja na kutajwa kuwa potovu na iliyopitwa na wakati.

You can share this post!

Macho yote kwa Shujaa,Morans Safari 7s ikianza

Usajili: Dada wa Raila awalaumu wanasiasa vikali

T L