HabariSiasa

Polisi wasaka wanaochochea ghasia za kikabila Twitter

January 10th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

IDARA ya Polisi imetangaza kuwa inawinda jamaa mmoja ambaye amekuwa akitumia mtandao wa Twitter kusambaza jumbe za kuchochea vurugu za kikabila nchini.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, NPS Alhamisi ilisema kuwa kuna mtu ambaye amekuwa akituma jumbe kuchochea vita vya kikabila kama vilivyoshuhudiwa baada ya uchaguzi wa 2007, ikisema anaandamwa.

“Tumevutwa na jumbe kadha kwenye twitter zilizochapishwa na mtu fulani akitoa vitisho kuchochea vita vya kikabila kama vilivyoshuhudiwa katika sehemu fulani za nchi 2007/8,” idara hiyo ikasema.

Iliendelea kusem kuwa inachukua hatua zote kuhakikisha kuwa vitisho vya aina hiyo havipuuziliwi, na kuwa wanaohusika watakabiliwa kisheria.

“Ifahamike kuwa tunachukulia vitisho hivi kwa uzito na tunashirikiana na NCIC kwa lengo la kukabiliana na watu wanaohusika na misingi ya kisheria,” polisi wakasema.

Ujumbe uliokuwa ukirejelewa ulilenga kushurutisha jamii fulani kuung kiongozi fulani wa kisiasa mkono katika uchaguzi ujao, ama ghasia ziibuke.