Polisi wasaka wanaotupa miili Yala

Polisi wasaka wanaotupa miili Yala

Na KENYA NEWS AGENCY

POLISI katika Kaunti ya Siaya wameimarisha doria kando mwa Mto Yala kwa lengo la kukomesha utupaji wa miili ya watu waliouwa kwingineko.

Kamanda wa polisi katika kaunti hiyo, Michael Muriithi alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuibuka kwa ripoti kwamba kuna watu ambao hutupa miili mtoni humo.

Akiongea na wanahabari mjini Siaya, Bw Muriithi alihakikishia umma kuwa maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) wanafanya kila wawezalo kupata ukweli kuhusu suala hilo.

Alisema wanashirikiana na wenzao kutoka kaunti jirani za Kakamega, Nandi na Uasin Gishu ili wafanye uchunguzi katika mito midogo inayoelekeza maji katika Mto Yala.

Mnamo Jumatatu, wakazi wa mji wa Yala walielezea hofu kuhusu ongezeko la idadi ya miili ambayo imekuwa ikipatikana imetupwa katika mto tangu mwaka jana. Miili 19 imeopolewa mtoni humo katika muda wa miezi mitatu iliyopita.

Kulingana na wakazi, nyingi za miili hiyo hupatikana karibu wa eneo la maporomoko ya maji la Ndanu.

Bw Nicholas Okero ambaye huopoa miili kutoka mto Yala alisema ameopoa miili 31 ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita.

“Baadhi ya miili huwa imewekwa ndani ya maguni yaliyoshonwa,” akasema Bw Okero.

  • Tags

You can share this post!

Chama chaomba mahakama itupilie mbali rufaa inayolenga...

TUSIJE TUKASAHAU: Mradi wa maji Nakuru haujakamilika kama...

T L