Habari

Polisi wasema mashahidi wa mauaji bado kupatikana, wataka muda zaidi

March 20th, 2020 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

POLISI bado hawajafanikiwa kuwapata wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Nairobi walioshuhudia mkasa ambapo inadaiwa mwenzao alipigwa kinyama na walinzi wa kampuni ya Lavington hadi akafariki wiki mbili zilizopita.

Makachero wanaochunguza kifo tatanishi cha mwanafunzi huyo Elisha Otieno maarufu kama ‘Ras’ Machi 4, 2020, walidai kwamba mashahidi hao hawajaandikisha taarifa kwa sababu imekuwa vigumu kuwapata.

Ugumu umetokea baada ya chuo hicho kufungwa kutokana na agizo la serikali la kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

“Sijafanikiwa kuwapata wanafunzi mashahidi ili waandikishe taarifa na bado hatujawahakikishia usalama wao jinsi inavyotakikana kisheria. Tangu kufungwa kwa chuo, imekuwa vigumu kuwapata,” akasema afisa wa cheo cha koplo Philip Bett katika Mahakama ya Milimani, Nairobi.

Afisa huyo wa upelelezi alikuwa amerejea mahakamani akiomba apewe muda zaidi wa kumzuilia mshukiwa wa mauaji hayo Spencer Kipkorir Kosgey kwa siku tano ili awafikie mashahidi hao.

Kosgey alinyakwa mnamo Machi 11 na makachero kutoka kituo cha polisi cha Kilimani na amekuwa akizuiliwa kituoni humo tangu wakati huo.

Inadaiwa kuwa ni mmoja wa walinzi waliomkamata marehemu kisha kudai walikuwa wakimpeleka katika kituo cha polisi cha Central.

Badala yake inadaiwa walimpelekea katika bustani ya Central ambako walimnyonga na kumpiga.

Siku iliyofuata msamaria mwema aliokoa Bw Otieno na kumpeleka katika hospitali ya Kenyatta ambako alifariki akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Uchunguzi wa maiti kwenye mwili wa marehemu uliofanyika Machi 11 katika hospitali ya Chiromo na mtaalamu wa upasuaji wa miili Peter Ndegwa, ulionyesha kwamba alipigwa kwa kifaa butu kichwani na kunyongwa.