Habari Mseto

Polisi washirikianao na wauzaji pombe motoni

February 3rd, 2020 2 min read

JUSTUS OCHIENG na VITALIS KIMUTAI

SERIKALI imelazimika kuchukua hatua ili kukomesha utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu na dawa zingine za kulevya, ambayo inalaumiwa kuwa imewaharibu vijana wengi pamoja na kuvunja familia.

Kwa kupitia waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i na katibu katika wizara hiyo Karanja Kibicho, serikali inapanga kutumia maafisa wa polisi wa kawaida, pamoja na wale wa utawala, kumaliza tatizo hili.

“Tunaanza juhudi za kukabiliana na uuzaji wa dawa za kulevya, najua itakuwa kazi ngumu, lakini tumejitayarisha kuanza hii safari,” Dkt Matiang’i akasema.

Waziri huyo alisema haya majuzi katika mkutano wa usalama, wakati maafisa wa polisi walioaminiwa kutekeleza mpango wenyewe wanaendelea kukinzana, na kushirikiana na wauzaji wa vileo hivyo haramu.

Katika Kaunti ya Homa Bay, baadhi ya maafisa wa polisi wanashirikiana na wafanyabiashara wa vileo hivyo kuendeleza biashara yenyewe, hali ambayo imelazimu wasimamizi wa serikali wa utawala kufanya misako bila kusaidiwa na polisi, wakihatarisha maisha yao.

“Tunapitia hatari sana kwani tunaweza kuvamiwa. Kwa sasa tunaenda peke yetu bila ulinzi wa polisi, kwani kila wakati tulipokuwa tukishirikiana nao hatukupata pombe haramu, kwa kuwa waliwafahamisha wafanyabiashara hao kuhusu msako hata kabla yetu kufika,” akasema mmoja wa maafisa ambao wamekuwa kipaumbele kukabiliana na pombe haramu kaunti hiyo.

Katika visa kadhaa, machifu na manaibu wao wamevamiwa wakati wanapofanya msako wa kutafuta pombe haramu, japo wizara ya usalama wa ndani inazidi kushikilia kuwa imejitolea kumaliza pombe hizo.

Polisi katika kituo cha kupiga doria cha Sindo, eneo la Suba wamelaumiwa vikali, kuwa walificha pombe haramu aina ya Chang’aa lita 140 ambayo ilikuwa imekamatwa na viongozi wa utawala eneo hilo, badala yake wakiweka maji.

Pombe hiyo ilikuwa sehemu ya lita 4,710 aina ya Kangara, ambayo ilipangiwa kuharibiwa wakati wa operesheni hiyo.

Operesheni hiyo iliongozwa na naibu kamishna wa kaunti eneo la wilaya ya kati, Abdullalahi Abdimalik pamoja na machifu, manaibu wao na wazee wa vijiji eneo hilo.

Inadaiwa polisi walificha pombe hiyo ili mshukiwa aliyekamatwa nayo, Vitalis Otieno, aachiliwe kwa ukosefu wa ushahidi.

Kamishna wa Kaunti ya Homa Bay David Kipkemei alisema malalamishi hayo yanachunguzwa na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kaunti hiyo.

“Ni kweli baadhi ya maafisa wa polisi walishirikiana na mshukiwa na kubadilisha lita 140 za Chang’aa na maji ili kukwepa korti lakini uchunguzi umeanzishwa na washukiwa watakamatwa,” Bw Kipkemei akasema.