Habari Mseto

Polisi washtakiwa kwa kuuuza pombe haramu

January 15th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

MAAFISA wawili wa polisi na mfanyabiashara moja wa kike, Jumatatu walikanusha mashtaka ya kujihusisha na biashara ya kuingiza vileo nchini kwa njia haramu.

Meshack Musembi na Harrison Kemboi, ambao ni polisi wa utawala wanaohudumu katika makao makuu ya Kaunti ya Kakamega, pamoja na mfanyabiashara Tabitha Ngera, walikamatwa mnamo Jumapili katika makutano ya Mayoni kwenye barabara ya Mumias-Busia wakati wa operesheni ya kunasa bidhaa ghushi.

Watatu hao walipatikana wakisafirisha sacheti 6,000 za vileo ndani ya gari la serikali la taifa jirani la Uganda ambapo walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Mumias.

Hata hivyo, jana walikanusha mashtaka manne ya kushiriki biashara haramu kinyume cha sheria mbele ya Hakimu Mkuu Mkaazi wa mahakama ya Mumias, Fredrick Nyakundi.

Katika mashtaka ya kwanza na ya pili, walilaumiwa kwa kusafirisha sacheti 5,760 za pombe aina ya Simba Waragi Gin na sacheti nyingine 240 za kileo chenye kahawa mtawalia.

Katika mashtaka ya tatu na nne walikumbana na hatia ya kumiliki aina hizo mbili za pombe.

Kiongozi wa mashtaka, Kaburu Makena alieleza mahakama kwamba watatu hao walikamatwa wakati wa operesheni hiyo na kupatikana na magunia 10 yaliyojaa sacheti 6,000 za pombe yenye thamani ya Sh200,000.

Washukiwa hao wote waliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini sawa na kiasi hicho cha pesa huku kesi hiyo ikiratibishwa kutajwa Januari 17, kisha kusikizwa Januari 27.