Habari Mseto

Polisi watano ndani kwa kuiba pombe

August 13th, 2020 1 min read

DICKENS WESONGA NA FAUSTINE NGILA

Polisi watano akiwemo OCS wa kituo cha polisi cha Boya ambacho kiko kaunti ndogo ya Nyando, Kisumu walilala ndani Jumatatu baada ya kukamatwa wakiiba pombe kutoka kwa lori liliopata ajali.

Kamanda wa polisi wa kaunti Ranson Lolmondong aliwatambua waliokamatwa kuwa OCS , Inspekta mkuu William Cheruiyot, Corporal Jane Chepkemei konstabo wa polisi Bernard Macharia, Sameel Maina na Rodrick Laushuset.

Alisema kwamba walikamatwa na wapelelezi wa DCI kutoka Nyando na wakapelekwa kwenye kituo cha polisi cha Ahero.

“Maafisa hao wamefungiwa huku kesi ikiendelea kuchunguzwa na maafisa wa DCI Kisumu,”alisema mkuu huyo wa polisi.

Ripoti kutoka afisi ya DCI zilisema kwamba maafisa hao walipatikana wakiiba pombe ya Vodka baada ya lori kupata ajali kwenye barabara ya Ahero-Awasi karibu na soko ya Boya.Hakuna watu waliumia kwenye ajali hio.

Maafisa hao wanasemekana kuiba pombe walipokua wakilinda lori hilo pamoja na wakazi waliokimbia eneo la tukio.