Habari Mseto

Polisi watatu kizimbani kwa kumtisha mfanyabiashara

April 16th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA watatu wa Polisi walifikishwa mahakamani na kuagizwa wazuiliwe kwa siku tano rumande wahojiwe kuhusiana na tuhuma za kushiriki kwa visa vya uhalifu.

Konstebo Oliver Tambo Mayavi, Kevin Brian Adanje na Duncan Waseke walifikishwa mbele ya hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe Jumanne.

Bi Nzibe alielezwa kuwa maafisa hao walimtia nguvuni mfanyabiashara Joe Gakure Muburi na kumsumbua sana na kumtisha.

“Bw Muburi alifika katika kituo cha polisi cha Central na kutoa ripoti kuwa maafisa watatu wa polisi aliowatambua kwa majina Konstebo Oliver Tambo Mayavi, Kevin Brian Adanje na Duncan Waseke wakiandamana na maafisa wengine wa polisi kutoka kituo cha Kamukunji na maafisa wa kitengo cha Flying Squad walimtia nguvuni na kumuweka pingu,” Sajini Joab Owino alimweleza Bi Nzibe.

Sajini Owino alisema maafisa hao wa polisi walizunguka wakiwa na mlalamishi kwa masaa mengi huku “wakimtisha kumfungulia mashtaka.”

Mahakama iliamuru polisi hao wazuiliwe kwa siku tano kusaidia katika uchunguzi.