Habari Mseto

Polisi wategua kitendawili cha vifo vya wawili ndani ya kanisa

July 17th, 2018 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

MAAFISA wa polisi katika Kaunti ya Kirinyaga wameeleza kuwa mwanamume na mwanamke ambao miili yao ilipatikana ndani ya kanisa wakiwa wamekufa waliuawa kwa kupewa sumu na kuzimiwa hewa.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa DCI Kitengo cha Mauaji eneo la Kirinyaga, Justus Kipyegon, wawili hao waliuawa kwa kunyweshwa kemikali ya methanol na kuzimiwa hewa kwa kuwekwa matambara midomoni.

Polisi sasa wanafuatilia habari kuwa sababu ya mauaji ya wawili hao yanahusu pesa ambazo mwanamke huyo, aliyetambuliwa kama Regina Kathure kutoka eneo la Mavuria, Kaunti ya Embu, alikuwa ameuza shamba siku chache kabla ya kuuawa.

Bw Kipyegon alisema walioua wawili hao walitaka ionekana kana kwamba walikuwa wakizini ndani ya kanisa, ndiposa Mungu akawaadhibu.

Alisema uchunguzi wao unaonyesha waliopanga mauaji hayo sio majambazi wa kawaida, lakini ni watu ambao walipanga njama hiyo kwa umakinifu mkubwa ili kuvuruga uchunguzi.

Miili ya wawili hao ilipatikana ndani ya kanisa la Holy Ghost Terbanacle katika eneo la Muringe, Kaunti ndogo ya Ndia mnamo Jumamosi. Kando mwa miili hiyo iliyokuwa uchi wa wanyama mlikuwa na mipira miwili ya kondomu iliyokuwa imetumika. Miili hiyo pia ilikuwa imelazwa kwa kukaribiana.

“Mwanamke huyo alikuwa ameuza shamba lake kwa Sh1.2 milioni. Alikuwa amelipwa Sh800,000 akingojea masalio baada ya kukamilisha shughuli ya kubadilisha hatimiliki,” akasema afisa hiyo.

Alieleza kuwa haijabainika uhusiano wake na kijana waliyeuawa pamoja ulikuwa upi: “Kuna uwezekano mkubwa kijana huyo alikuwa ametumwa na waliopanga mauaji hayo kufuatilia mienendo ya Bi Kathure na alipofanikisha njama hiyo akauawa pia ili kumzima asiwasaliti.”

Bw Kipyegon aliongeza kuwa uchunguzi wa kina ambao tayari umetekelezwa umebaini kuwa mipira hiyo ya kondomu haikuwa imetumika ndani ya kanisa hilo kwa kuwa vipakio vyake havikuwa katika eneo hilo.

“Kuna uwezekano mkuu kuwa waliotekeleza mauaji hayo walisafiri na mipira hiyo kutoka kwingine. Uchunguzi umebaini kuwa mwanamke huyo hakuwa ameshiriki ngono kama ilivyokuwa ikidhaniwa awali,” akasema.

Miili hiyo pia ilikuwa imepanguzwa kwa kitambaa ili kuondoa alama zozote za vidole.

Alisema simu ya mwanamke huyo imetwaliwa na maafisa wanaochunguza mauaji hayo na wamegundua kuwa alikuwa safarini kuelekea Nairobi, na kuna uwezekano walitekwa nyara wakitafuta usafiri au lojing’i katika mji wa Kagio.

Bw Kipyegon alisema kuwa kuna washukiwa wanne ambao walikuwa wamenaswa Jumapili lakini waliachiliwa baada ya kukosekana ushahidi wa kuwahusisha na mauaji hayo.

Alisema kuwa hizo zote ni njama za wauaji halisi za kukwepa mtego wa uchunguzi ambapo katika kila awamu ya hila zao, walikuwa wakihakikisha wamefuta ushahidi.

Alisema kuwa visa vya watu kuuawa katika Kunti ya Kirinyaga kuhusiana na masuala ya mashamba limekuwa jambo la kawaida.

“Lakini bado tunafuatilia kisa hiki na tayari tumewasiliana na wenzetu kutoka Embu ili watupekulie zaidi kuhusu aliyekuwa ameuziwa shamba na waliokuwa mashahidi katika mauzo hayo,” akasema.

Wakati huo huo, maombi ya kutakasa kanisa hilo yaliandaliwa jana jioni yakiongozwa na Askofu Peter Mburu, ambaye ndiye Mkuu wa makanisa hayo Mlima Kenya.

Askofu Mburu ndiye pia alitakasa kanisa la PEFA la Gakira, Kaunti ya Murang’a mnamo 2007 baada ya kundi haramu la Mungiki kuua dereva na makanga ndani ya kanisa hilo kwa kuwakata vichwa.

Mnamo Jumapili, Afisa Mkuu wa Polisi wa Utawala wa eneo hilo, Boniface Mwaniki alisema wenda zao walikuwa wameonekana awali katika mji wa Kagio wakinywa pombe pamoja, na walitoka baa walimokuwa mwendo wa saa nne usiku.

Alieleza kuwa taarifa za mashahidi waliowaona wawili hao wakitoka baa hiyo zinaonyesha kuwa walitembea kuelekea barabara ya Makutano – Sagana.

Bw Mwaniki alisema kuwa kanisa hilo ambalo limejengwa kwa mbao na mabati lilikuwa limevunjwa kufuri ya mlango.

“Nje ya kanisa hilo kulikuwa na alama za magurudumu ya pikipiki. Licha ya mmiliki wa baa walimokuwa wakibugia pombe kusema kuwa alikuwa amewapa wawili hao chenji ya Sh450 walipokuwa wakitoka, hakuna pesa zilizokuwa katika eneo hilo la mauti,” akasema Bw Mwaniki.

Alieleza kuwa miili hiyo ilipelekwa katika mochari ya Embu kuhifadhiwa huku uchunguzi zaidi ukiendelezwa.

“Kwa sasa, tumechukua alama za vidole za miili hiyo na pia mipira ya kondomu ili kuchunguza kama uchafu ulio ndani yazo ni wa ngono ya wawili hao au ni wa mwingine,” akasema.

Alisema kuwa uchunguzi zaidi utatekelezwa katika upasuaji wa miili ili kufahamu jinsi walivyoaga.