Polisi watibua maandamano ya wafuasi wa Bobi Wine jijini Nairobi

Polisi watibua maandamano ya wafuasi wa Bobi Wine jijini Nairobi

 

MERCY CHELAGAT Na SAMMY WAWERU

Maafisa wa polisi Ijumaa walifurusha kundi la wafuasi wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine katika bustani ya Jeevanjee, Nairobi, waliopanga kuandaa maandamano jijini kushinikiza Rais Yoweri Museveni kujiuzulu.

Maafisa hao waliokuwa na gesi ya vitoa machozi, walinyang’anya kundi hilo mabango kabla kuanza maandamano.

Kundi hilo lililojumuisha raia wa Uganda wanoishi hapa nchini Kenya lilipania kuandamana kuanzia bustani Jeevanjee hadi katika afisi za ubalozi wa Uganda, zilizoko Riverside.

Walisema lengo lao lilikuwa kuwasilisha malalamishi ya kutoridhishwa na uchaguzi wa Uganda uliofanyika juma lililopita. Aidha, walidai shughuli hiyo haikuwa ya uhuru na haki.

Kundi hilo lilisema mgombea wa chama cha NUP, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, alipokonywa ushindi wake, kufuatia uchaguzi uliofanyika mnamo Januari 14, 2021.

Rais Museveni, 76, aliibuka mshindi na kuweza kuhifadhi kiti chake. Ametawala Uganda kwa muda wa miaka 34, tangu 1986.

Bobi Wine pia anadai kuwa alipokonywa ushindi, na amepanga kuelekea mahakamani.

Rais Museveni (NRM) hata hivyo anasisitiza uchaguzi huo haukukumbwa na udanganyifu wa kura.

Naibu kamanda wa polisi kaunti ndogo ya kati, Nairobi, Bw Mbusa Awuor alisema hakupokea notisi yoyote ya maandamano ya kundi hilo, huku akiyataja kama “maandamano haramu”.

Hata hivyo, barua iliyotazamwa na Taifa Leo Dijitali, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Nairobi alikuwa amearifiwa kuhusu maandamano hayo mnamo Januari 19.

Aidha, barua hiyo pia ilitumwa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kati, jijini Nairobi.

Bob Njagi kutoka Haki Africa aliambia wanahabari: “Tuliarifu kamanda wa polisi. Isitoshe, tumepigiwa simu kutoka afisi ya Rais kutaka kujua sisi ni kina nani na lengo letu. Hatuna shida na serikali ya Kenya na tumefuata mikakati ifaayo kisheria.”

Alipoulizwa kuhusu barua hiyo iliyokuwa na muhuri wa kamanda mkuu, Bw Awuor hakutoa majibu.

Baadhi ya watu waliokuwa wakijituliza katika bustani ya Jeevanjee walikosoa hatua ya kundi hilo, wakilitaka kuondoka ili kutovuruga utulivu wao.

Mwanaharakati Anthony Muraya hata hivyo alisema raia hao wa Uganda wana haki kutetea uhuru wa demokrasia. “Wanataka demokrasia katika nchi yao. Umewadia wakati mambo yabadilike kuwa bora,” akasema.

Bw Muraya pia alidokeza kwamba watajipanga na kuungana tena, kujua mwelekeo mwingine.

“Tutaandaa na kufanya maandamano mengine juma lijalo. Tutashangaza maafisa wa polisi,” akasema mwanaharakati huyo.

Alhamisi juma lililopita, Mkurugenzi Mkuu wa Haki Africa, Bw Hussein Khalid pamoja na wanaharakati wengine walikamatwa wakati wakifanya kikao na wanahabari kushikiniza kuheshimiwa kwa demokrasia Uganda.

Baada ya matokeo ya uchaguzi Uganda kutolewa rasmi na tume ya uchaguzi nchini humo, Bobi Wine ameendelea kuhangaishwa na serikali ya Museveni, huku wanajeshi wakizingira makazi yake na kumzuia kutoka.

 

You can share this post!

KALONZO ABURUTA RUTO TOPENI

Kenya yasifiwa kutumia teknolojia kuzuia kuenea kwa corona...