Habari Mseto

Polisi watibua uwezekano wa machafuko kuhusu ardhi Murang'a

February 14th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

POLISI wa Utawala Alhamisi walilazimika kuingilia kati mgogoro wa ardhi kati ya pande mbili eneo la Kihumbu-ini, kijiji cha Gathinji, Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

Taharuki ilitanda pale maafisa wa ardhi kutoka Thika, walipofika eneo hilo ili kutatua mzozo huo wa ardhi.

Msajili wa ardhi mjini Thika Bw Robert Mugendi, na soroveya Bw O. Franklin, walijipata njia panda wakizuiliwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Maafisa hao walizuru eneo hilo ili kujua hasa ukweli wa mambo, kwani wanakijiji katika eneo hilo walizua vurugu wakiwataka wawili hao wasiingilie maswala hayo.

Lengo lao kuu lilikuwa ni kukagua eneo hilo kama kweli lilikuwa linazozaniwa na pia kuhakikisha wametuliza joto hilo la kung’ang’ania ardhi.

Mkazi wa kijiji hicho Bw Samuel Karungo Kihara alikuwa na mvutano wa ardhi na majirani wake sita wa kijiji hicho na hapo ndipo mzozo ulipotokea.

Kabla ya polisi kutoka kwa gari lao, taharuki ilikuwa imetanda kote huku vikundi viwili pinzani vikiwa tayari kukabiliana kwa silaha. Picha/ Lawrence Ongaro

Hata hivyo mmoja wa majirani hao alipinga mambo hayo akiyataja kama propaganda tupu.

Polisi hao walilazimika kujiweka katikati ili kutuliza purukushani hiyo lakini bado mambo yalikuwa ya kutatanisha.

Hata hivyo baada ya maafisa wa ardhi kusikiza malalamiko hayo walilazimika kuwapa wakati wa kuzuru afisi za ardhi mjini Thika mnamo Februari 26, 2019, ili pande zote ziwasilishe stakabadhi zao mezani ili kutambua msema kweli ni nani.

Ardhi inayozozaniwa ni ya ekari 2.6 na ilisemekana punde pande zote mbili zitaleta  stakabadhi zao siku iliyotajwa bila shaka ukweli utajulikana.

Chifu wa eneo hilo Bw Francis Kamau Mungai aliwaonya wakazi hao wasiendelee kuchochea wengine bali wangojee hadi uamuzi kamili utatolewa tarehe iliyotajwa.