Habari Mseto

Polisi watumbua jipu la ulanguzi wa binadamu Nairobi, waokoa raia 79 wa kigeni

November 19th, 2018 1 min read

Na MWANDISHI WETU

MAAFISA wa polisi Ijumaa waliwaokoa raia 79 wa kigeni kutoka kwa walanguzi wa binadamu mtaani Mlango Kubwa, Kaunti ya Nairobi.

Maafisa hao kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walitua katika mtaa huo katika eneo bunge la Starehe baada ya kudokezewa na wananchi kuhusu kuwepo kwa raia wa kigeni.

Waliopatikana walikuwa raia 75 wa visiwa vya Komoro, watatu wa Uganda na mmoja wa Congo ambao walikuwa na umri wa miaka kati ya 19 na 45, waliokuwa wamewekwa bila hiari yao.

Polisi walisema raia hao kwa sasa wamo mahali salama. “Makachero tayari wameanza uchunguzi kubaini waliohusika katika uhalifu huu,” DCI ilisema.

Ripoti ya 2018 kuhusu ulanguzi wa watu ilitaja Kenya kama kitovu cha visa vya ajira za kulazimishwa na ulanguzi wa watu wanaofanywa mateka wa ngono, katika kanda ya Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo ya 2018 ya Ustawi wa Kiuchumi Afrika ilitayarishwa na Muungano wa Afrika (AU).