Habari

Polisi watumia vitoa machozi kutibua mkutano wa Mumias

January 18th, 2020 1 min read

DERICK LUVEGA na SHABAN MAKOKHA

POLISI wamerusha gesi Mumias kuwazuia wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto kuandaa mkutano wao mbadala wa ule wa Jopo la Maridhiano (BBI) unaofanyika leo Jumamosi katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega.

Matukio ya polisi wakikabiliana na wanaoegemea mrengo wa Ruto yameshuhudiwa katika maeneo ya Ekero na Shibale mjini Mumias, Kaunti ya Kakamega ambapo walirusha mikebe ya gesi ya kutoa machozi na hivyo kuzima juhudi za viongozi kuhutunia na hata kuhudhuria mkutano katika uwanja wa Nabongo walioratibu kuukabili ule wa BBI.

Mkutano wao wa Nabongo ulifutwa na vyombo vya usalama.

Makabiliano hayo yalishuhudiwa dakika chache baada ya viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa na Seneta wa zamani wa Kaunti ya Kakamega Dkt Boni Khalwale, kushutumu maafisa wa polisi kuhusu kutoweka kwa Mbunge wa Mumias Mashariki Ben Washiali ambaye alitarajiwa kuwaongoza katika kile walitaja ni mkutano wa kuangazia jinsi ambavyo wanaweza kukwamua eneo pana la Magharibi hasa kujiinua kiuchumi.

Maafisa walitawanya umati uliokuwa eneo la Ekero, Mumias ukihutubiwa na Bw Echesa.

Viongozi wengine waliokuwepo ni mbunge Justus Murunga (Matungu), John Walukhe (Sirisia), Didmus Barasa (Kiminini), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), na Charles Gimose (Hamisi).

Hali hiyo imelazimu hadhira kutawanyika.

Viongozi hao walifululiza hadi Shibale nao maafisa wakiwakabili.

Katika daraja la Mto Nzoia lililopo baina ya Ekero na Shibale, polisi walilazimika kuondoa kwa kuzima moto uliowashwa katikati ya barabara ya Mumias-Bungoma.

Viongozi hao wamesema wataandaa mkutano wao wikendi ijayo.

Mbunge wa Matungu Justus Murunga amesema walikuwa wamenuia kutumia nkutano wao huo mbadala kudhihirisha wao si waoga.