Habari Mseto

Polisi waua jambazi sugu aliyejaribu kuwashambulia kwa kisu

October 1st, 2020 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

POLISI kaunti ya Lamu wamempiga risasi na kumuua papo hapo mwanamume jambazi aliyejaribu kuwatisha maafisa hao kwa kisu na bunduki ya muigo.

Mwanamume huyo Fadhil Muhidin,25 alipigwa risasi baada ya kukataa kusalimu amri ya kukamatwa.

Mwanamume huyo alikuwa awali amevamia duka moja na kumuibia mmiliki wa duka hilo mtaani Gadeni kisiwani Lamu kima cha fedha kisichojulikana.

Baadaye alikimbia na kujitupa baharini na kuogelea kwa karibu kilomita moja akijaribu kuwatoroka polisi.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Moses Murithi alisema maafisa wake walitumia boti kumfukuza mwanamume huyo, ambapo walipojaribu kumkamata alitoa bunduki bandia na kisu na kuwatisha maafisa hao kwamba angewashgambulia.

“Hapo ndipo mmoja wa maafisa wetu alitoa bunduki na kumpiga risasi katika harakati za kumzuia asiwazuru. Bahati mbaya risasi ilimuua. Mwili wake umepelekwa kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali ya King Fahad mjini Lamu ukisubiri upasuaji,” akasema Bw Murithi.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia pia alithibitisha kisa hicho na kuwataka wananchi kutii sheria.

Bw Macharia alisema hadi kifo chake, mwanamume huyo amekuwa akitumbukizwa gerezani kwa kushiriki uhalifu wa kila mara.

“Ni jambazi ambaye kila mara amekuwa akishiriki uhalifu. Alikuwa ameachiliwa miezi miwili iliyopita kutoka gerezani lakini tulikuwa tukipokea habari kwamba amekuwa akiwatisha raia kila mara. Zake arobaini zimemfikia leo,” akasema Bw Macharia.

Tukio hilo linajiri mwezi mmoja baada ya polisi eneo hilo kumuua mwanamume kwa jina Bunu Sabaki Shee,30 katika kijiji cha Kwasasi baada ya jaribio lake la kuwashambulia maafisa hao wa upanga kutibuka.

Mapema Agosti mwaka huu, polisi eneo la Siyu, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki pia walimpiga risasi na kumuua papo hapo mwanamume mwingine aliyekuwa katika harakati za kuwashambulia maafisa wa polisi majira ya jioni.