Habari Mseto

Polisi waua watu watatu uchaguzi ukianza Tanzania

October 28th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

CHAMA kikuu cha upinzani katika kisiwa cha Zanzibar kisichojisimamia binafsi, kilisema jana kuwa watu watatu waliuawa na polisi katika Kisiwa cha Pemba, huku ghasia zikizuka siku moja kabla ya uchaguzi nchini Tanzania kung’oa nanga leo.

Polisi waliripotiwa kufyatua risasi na kuua kikatili kijana mmoja katika ngome ya upinzani ya Garagara, huku vikosi vya usalama vikianza kupiga kura siku moja kabla ya uchaguzi wa urais na ubunge.

Kambi ya upinzani inaamini kuwa siku maalum ya upigaji kura mapema ni njama ya kuiba kura katika kisiwa hicho chenye historia ya chaguzi zinazozozaniwa na kuapa kushiriki upigaji kura siku hiyo vilevile.

Machafuko yalizuka katika Kisiwa cha Pemba, ambacho ni ngome ya upinzani huku jeshi likisambaza visanduku vya kura ambavyo wafuasi wa upinzani waliamini vilikuwa vimetiwa alama hapo awali.’Ripoti zilizothibitishwa kutoka Pemba, Zanzibar, zinaashiria kuwa raia watatu wamepigwa risasi na polisi,” ilisema taarifa kutoka chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo (Alliance for Change and Transparency).

Chama hicho kilitaja watu watatu waliofariki pamoja na wengine watatu waliojeruhiwa.’Tunatoa wito kwa jamii ya kimaeneo na kimataifa kushawishi serikali za Tanzania na Zanzibar kuruhusu uchaguzi huru na wa haki kuendeshwa pasipo dhuluma za kikatili na vitisho katika kipindi cha wiki mbili zijazo.”

Kulikuwa na idadi kubwa ya polisi na wanajeshi kote katika visiwa hivyo.Katika eneo la Garagara, ambapo kiongozi wa upinzani Seif Sharif Hamad alitarajiwa kupiga kura, polisi wa kuzima ghasia walikimbia mitaani wakifyatua risasi na vitoa machozi.

Kundi la maafisa wapatao sita walimpa kichapo bila huruma kijana mmoja kwa kutumia bunduki na fimbo zao, kabla ya kumtupa nyuma ya gari lao, nao wanahabari wakifukuzwa kutoka eneo hilo.Chama cha ACT Wazalendo kilisema mwaniaji wao wa urais Zanzibar ni Maalim Seif Sharif Hamad.

Afisa mmoja wa polisi jijini Zanzibar, Mohammed Hassan Haji, alithibitisha kukamatwa huko kwa vyombo vya habari lakini hakutoa maelezo yoyote ya kina.

Hata hivyo, polisi jijini Pemba hawakusema lolote kuhusu madai ya ACT Wazalendo kwamba polisi waliwapiga risasi na kuwaua watu watatu na kuwajeruhi wengine wapatao tisa mnamo Jumatatu jioni usiku wa kuamkia upigaji kura eneo hilo.

“Leo usiku jeshi limekuwa likisambaza visanduku vya kura,” taarifa ya chama hicho ilisema.