Habari

Polisi wazidi kukaidi amri za kafyu

April 18th, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

MAAFISA wa polisi wanaonyesha mfano mbaya kwa kuwa mstari wa mbele kukaidi kanuni zilizowekwa na Wizara ya Afya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Katika muda wa wiki tatu, zaidi ya maafisa 30 wamekamatwa kwa kukiuka sheria, kutumia nguvu kupita kiasi na kupokea hongo wakitekeleza maagizo ya serikali ikiwemo amri ya kutotoka nje usiku.

Mnamo Alhamisi, Rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba, ingawa maafisa wa usalama wanatekeleza jukumu muhimu wakati huu wa kukabiliana na corona, wale wanaovunja sheria au kusaidia watu kuvunja sheria hawatavumiliwa.

“Kila wakati kanuni zinapo vunjwa kwa usaidizi wa maafisa wa serikali, huwa ni kuhatarisha maisha ya Wakenya. Afisa yeyote atakayehatarisha maisha ya Wakenya wakati wa janga hili atachukuliwa hatua kali zaidi,” alisema Rais.

Lakini licha ya onyo hilo, vitendo vya maafisa wa usalama vinafanya waonekane kama wao ndio sheria yenyewe. Polisi wamekuwa wakikamatwa wakilewa ndani ya baa baada ya saa moja usiku, wakati ambao wanapaswa kuhakikisha watu wote wako nyumbani.

Baa zote zinapaswa kufungwa kuanzia saa moja lakini imeibuka kuwa maafisa wa usalama wamekuwa wakisaidia wauzaji wa pombe kuuza baada ya saa moja jioni.

Katika kisa cha hivi punde, maafisa wawili wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Ematiha, Navakholo kaunti ya Kakamega, waklkamatwa na umma wakipokea hongo kutoka kwa wauzaji wa chang’aa. Wawili hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi wakisubiri kufikishwa kortini.

Katika kaunti ya Mombasa ambayo ni ya pili katika orodha ya maeneo yaliyo na visa vingi vya maambukizi ya corona, maafisa wawili wa vyeo vya juu katika idara ya magereza walikamatwa wakilewa katika baa moja eneo la Majaoni.

Wawili hao pia wanasubiri kufikishwa kortini kushtakiwa kwa kukiuka sheria ya afya ya umma na kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Mnamo Jumatano, maafisa watatu wa jeshi la Kenya, akiwemo mmoja wa cheo cha kanali, walikamatwa wakilewa katika baa moja eneo la Embakasi, Nairobi na kukabidhiwa idara ya nidhamu ya jeshi kuadhibiwa. Katika eneo hilo, hakimu wa mahakama alikamatwa pia akilewa kinyume na sheria za kuzuia kusambaa wa corona.

Katika eneo hilo, afisa wa kikosi cha ulinzi cha rais, alikamatwa Jumapili kwa kukiuka kafyu lakini akaachiliwa kufuatia agizo kutoka kwa wakubwa wake. Ripoti ya polisi inasema, afisa huyo wa cheo cha supritenda alikamatwa mwendo wa saa nne usiku.

Kukamatwa kwa maafisa hao kulijiri siku moja baada ya wengine saba wa polisi kupatikana katika baa iitwayo Maximum mtaani Bahati, Nairobi walikojifungia kulewa usiku.

Mkuu wa polisi eneo la Nairobi, Bw Philip Ndolo alisema walikamatwa kufuatia malalamishi kutoka kwa umma. Maafisa wanasema kuna uwezekano kwamba, wakuu wa polisi wamekuwa wakificha vitendo vya ukiukaji wa sheria vinavyotekelezwa na walio chini yao wakati huu wa kafyu na utekelezaji wa kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Katika eneo la Mwimto, Nairobi, afisa wa polisi alikamatwa kwa kushukiwa kuvunja duka na kuiba mali usiku akitekeleza kafyu. Afisa huyo alipatikana na mali iliyoibwa kutoka duka hilo.

Visa vya maduka kuvunjwa wakati wa kafyu vimekuwa vikiripotiwa kote nchini. Katika kaunti ya Siaya, afisa wa polisi wa cheo cha juu alikamatwa akilewa katika baa moja mjini Sega akiwa na watu wengine sita na mwingine akatiwa mbaroni kaunti ya Turkana kwa kupigana na wenzake waliokuwa wakitekeleza kafyu.

Katika kisa kilichoibua hisia kali miongoni mwa Wakenya, afisa wa polisi alirekodiwa kwenye video akitisha wanabodaboda waliokuwa wakisafirisha makaa walipokataa kumpa hongo kaunti ya Kwale. Afisa huyo alisimamishwa kazi baada ya kanda hiyo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Inaonekana Wakenya wamekuwa wakitii sheria kuliko maafisa wa polisi. Katika visa kadhaa, raia wamelazimika kuchukua hatua kulalamika kwenye mitandao ya kijamii au kwa wakubwa wa polisi,” asema wakili Samuel Nyariki.

Huko Nakuru, maafisa wanne wa polisi walisimamishwa kazi kwa kuwapiga watu wawili walipokuwa wakishika doria kuhakikisha kafyu imetekelezwa.

Katika kisa kilichokashifiwa na Wakenya, chifu mmoja katika kijiji cha Kaplelach kaunti ya Uasin Gishu alichukua sheria mikononi na kumwagia nyanya mmoja pombe ya busaa aliyodaiwa alikuwa akiuza.